Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MOLLEL AWAPONGEZA NTLP, NASHCOP KWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA WELEDI.

Posted on: August 27th, 2024


Na WAF - Dodoma,

Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel leo tarehe 27 Agosti, 2024 amekutana na watumishi wa Programu kutoka Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP) pamoja na Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) katika ofisi za Wizara ya Afya zilizopo kilimani jijini Dodoma.

Akiwa katika kikao kazi hicho ambacho Dkt. Mollel aliambatana na Naibu Katibu Mkuu Bw. Ismail Rumatila na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt, Ahmed Makuwani amewapongeza watumishi wa Programu hizo chini ya Mkuu wa Programu Dkt. Catherine Joachim kwa kutekeleza vizuri shughuli za kupambana na magonjwa hayo nchini.

Pia Dkt.Mollel, amewataka watumishi wa Programu kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa weledi mkubwa ili kuleta tija na ufanisi katika kufikia malengo ya nchi ya kutokomeza magonjwa hayo.

Kikao hicho kiliitishwa kwa lengo la kupokea taarifa za utekelezaji na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu udhibiti wa magonjwa hayo nchini.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Bw. Rumatila amewapongeza watumishi wa Programu hizo kwa kuwa na jitihada za kupambana na magonjwa hayo pamoja na kuwataka watumishi hao kuongeza kasi katika kuwatafuta wagonjwa wanaokosekana na kuwaweka kwenye matibabu ili kuzuia kuenea kwa magonjwa haya katika jamii.

Kwa upande wake Dkt. Catherine Joachimu amewashukuru viongozi hao kwa kutenga muda na kukutana na watumishi wa Programu hizo hatua ambayo itaongeza hamasa na chachu kwa watumishi katika kutekeleza mikakati ya nchi ya Kutokomeza magonjwa hayo ifikapo mwaka 2030.