Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. MOLLEL ACHANGISHA MILIONI 382 KUGHARAMIA UJENZI CHUO KIKUU KIGOMA

Posted on: May 25th, 2025

Na WAF-Dar es Salaam 


Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, leo Mei 25, 2025 amechangisha Shilingi Milioni 382 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kigoma akiwa amemuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango.



Dkt..Mollel amefanya zoezi hilo wakati uzinduzi wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Heri, mkoani Kigoma, ikiwa ni sehemu ya upanuzi katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Heri mkoani humo.


Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mollel amesema uwepo wa chuo hicho mkoani Kigoma ni chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa mkoa huo. 


Naibu Waziri Mollel amesema kuwa, chuo hicho kitakuwa daraja muhimu la kuongeza idadi ya wataalam wa afya nchini, jambo ambalo linaenda sambamba na dira ya Serikali ya kuboresha huduma za afya na kukuza elimu ya sayansi kwa manufaa ya taifa.


Aidha, Dkt. Mollel amesisitiza umuhimu wa mashirika na taasisi mbalimbali kuendelea kuunga mkono juhudi hizo siyo tu Kigoma bali pia katika maeneo mengine nchini.


"Hii siyo tu harakati ya Kigoma, bali ni harakati ya Taifa zima kuhakikisha tunarithisha vizazi vijavyo misingi imara ya elimu bora. Tuwe mabalozi wa maendeleo na tusimame pamoja kuhakikisha urithi huu wa elimu unaendelea kuwepo na kuleta tija katika jamii yetu." amefafanua Dkt. Mollel.


Dkt. Mollel ameongeza kuwa hatua ya kuanzisha chuo kikuu ni ishara ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuondoa changamoto ya vijana kusafiri umbali mrefu kufuata elimu ya juu huku akibainisha kuwa uwekezaji katika elimu ni moja ya njia bora za kupambana na umasikini, kukuza ujuzi, na kuboresha afya za wananchi kupitia wataalamu waliobobea.


Mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu unatarajiwa kusaidia siyo tu wakazi wa Kigoma, bali pia wanafunzi kutoka mikoa ya jirani na nchi za Maziwa Makuu, hivyo kuifanya Kigoma kuwa kitovu cha elimu ya afya na sayansi kwa kanda hiyo.