Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. KWESI AHITAJI USHIRIKIANO ILI KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: January 30th, 2024

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Njombe Dkt. Gilbet Kwesi, amewataka watumishi wa hospitali hiyo kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuboresha huduma na maslahi yao na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wakati wa kuwahudumia wananchi.

Dkt. Kwesi ametoa wito wakati alipofanya kikao na watumishi wote ambapo amasema baada ya kikao hicho anatarajia kuona mabadiliko ya utendaji kazi, hasa katika kuwahudumia wananchi wanaofika katika Hospitali hiyo.

“Ili twende vizuri, ni lazima tuzingatie muda wa kufika kazini, changamoto ya usafiri ni kubwa, lakini tutaangalia namna ya kuitatua na kupunguza kero kwa watumishi”, ameeleza Dkt. Kwesi

Vile vile amesema kila mtumishi katika hospitali hiyo aone sehemu atakayoboresha katika utendaji kazi wake ili kuleta ufanisi mzuri wa kuwahudumia wananchi.

Dkt. Kwesi ameongeza kuwa atatanua wigo mpana wa huduma za upasuaji ambapo amesema kuwa atahakikisha anaongeza idadi ya vyumba vya upasuaji na maeneo rafiki kwa huduma hiyo, huku jengo la Utawala likibaki kwa shughuli za Kliniki za wagonjwa wa nje na za kibingwa, Utengamao na Huduma za Mionzi.

“Tutakuwa na huduma malumu kwa kuwa na huduma ya FastTrack(huduma ya haraka kwa mteja na kwa daktari anayetaka amhudumie) na Wodi Binafsi itakayoenda sambamba na uboreshaji wa vyumba vya kutolea huduma hizo.

Kama watu watafanya kazi kwa bidii na wakazalisha wakavuka malengo, tutaanzisha kitu kinaitwa (Pay for Performance) yaani kulipwa kwa kadri ya uwajibikaji na uzalishaji wako, ili kuongeza motisha mahali pa kazi. Tufanye Outreach (kwenda kwa jamii) tukajue matatizo yao na tuwalete hapa wapate suluhisho la matatizo yao” amesema Dkt. Kwesi.