Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. JINGU ASHIRIKI KIKAO CHA 52 CHA BODI YA MFUKO WA DUNIA.

Posted on: November 21st, 2024

_Ashiriki kama Mjumbe akiwakilisha Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika (ESA)_

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ameshiriki kikao cha 52 cha Bodi ya Mfuko wa Dunia (52nd Global Fund Board) ambacho kinajadili hatua za kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa ya Kifua Kikuu, Malaria na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

Kikao hicho kimeanza Novemba 17, 2024 mjini Lilongwe nchini Malawi washiriki wakiwa ni wanachama 20 wanaopiga kura na wanane wa ziada wasiopiga kura kutoka nchi mbalimbali barani Afrika.

Kikao hicho kitakachohitimishwa Novemba 22, 2024 pia kitajadili mchango wa Mfuko wa Dunia kwenye masuala ya haki za binadamu na usawa wa kijinsia, mabadiliko ya tabia nchi na afya, uwekezaji, uendelevu na sera ya ufadhili wa pamoja.

Bodi ya Mfuko wa Kimataifa hukutana mara mbili kwa mwaka na Dkt. Jingu anashiriki kikao hicho kama Mjumbe wa kuchaguliwa wa Bodi hiyo akiwakilisha Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika (Eastern and Southern Africa - ESA).