Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DHARURA ZAIDI 60,000 ZASAFIRISHWA KUPITIA MFUMO WA M-MAMA

Posted on: March 25th, 2024Na WAF - Dodoma

Imebainishwa kuwa tokea kuanza kwa mfumo wa rufaa wa M-mama umehudumia dharura zaidi ya 60,000 kwa wanawake wajawazito, waliojifungua pamoja na watoto wachanga waliokua na uhitaji.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko Machi 25, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa kwanza wa kimataifa wa afya ya msingi pamoja na uzinduzi wa namba maalum ya dharura ya afya ya M-mama (115) ambayo imeanza kutoa huduma kwa dharura za wajawazito, waliojifungua na watoto wachanga.

"Kwa sasa rufaa zinazotolewa kituo kwa kituo zinafika dharura zaidi ya 5,500 kila mwezi ikiwa ni sawasawa na dharura 200 kila siku na dharura 8 kila saa nchi nzima". Amesema Dkt. Biteko.

"Hii inaonesha uhitaji mkubwa sana wa usafiri wa dharura kwa wajawazito, walojifungua na watoto wachanga ikiwa ni sehemu ya utoaji huduma bora za afya kwa wananchi popote walipo". Amesisitiza Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa mfumo wa M-mama unaratibiwa katika Hospitali za Mikoa kwa waratibu kupewa mafunzo ambapo namba 115 hutumika kutoa taarifa na waratibu hao kutoa huduma.

"Kazi kubwa sana imefanyika ndani ya mwaka mmoja, na sasa m-mama inapatikana kila mahali nchini. Nchi nyingine katika ukanda huu zimeendelea kujifunza toka Tanzania na kuanza kutekeleza mfumo huu wa dharura nchini kwao, ikiwemo Lesotho, Kenya na Malawi.

Akifafanua zaidi amesema Mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, Serikali ya Nigeria ilikuja Tanzania kujifunza mikakati tunayoitumia kukokoa Maisha ya mama na mtoto ikiwemo huduma ya m-mama na serikali iliwapokea vizuri". Amesema Dkt. Biteko.

Aidha, amewashukuru wadau wa maendeleo Vodacom Tanzania, Vodafone Foundation, USAID, Benki ya Dunia na wadau watekelezaji wa mfumo Touch Health na Pathfinder International kwa mchango wao katika kushirikiana na serikali kuleta huduma hii.

Naye Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel akitoa salaam za Wizara, amewashukuru wafanyakazi wa afya nchini kwa kujitolea kuboresha huduma za afya ambapo kupitia wao idadi ya vifo vya akinamama wajawazito vimepungua kutoka 556 hadi 104 mwaka 2023.