Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DAWA ZINAZOTUMIKA SANA NA WAZEE KUANZA KUTOLEWA MPAKA NGAZI YA ZAHANATI

Posted on: May 30th, 2023

Na WAF, Bungeni Dodoma.

NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amebainisha kuwa, katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa dawa za wazee, Serikali imekuja na mkakati wa kuhakikisha dawa ambazo zinatumika sana na wazee zianze kutolewa mpaka ngazi ya Zahanati ili kuondoa changamoto hiyo.

Dkt. Mollel amesema hayo leo Mei 30, 2023 wakati akijibu swali la Mbunge wa Tabora mjini Mhe. Emmanuel Adamson Mwakasaka katika kikao cha 36 Mkutano wa kumi na moja, Jijini Dodoma.

"katika kukabiliana na ukosefu wa Dawa kwa Wazee, Serikali imeamua dawa ambazo zinatumika sana na Wazee zilizokuwa hazitolewi kwenye vituo vya Afya na Zahanati zianze kutolewa katika ngazi hizo." Amesema Dkt. Mollel.

Ameendelea kusema, Serikali imewajengea uwezo watumishi wa vituo vya kutolea huduma za afya ili kuweza kufanya maoteo halisi kulingana na mahitaji ya Dawa ya vituo husika na mazingira ya eneo husika.

Aidha, Dkt. Mollel amesisitiza kuwa, Bima ya afya kwa wote ndio suluhu ya kudumu ya kupata huduma za matibabu bila gharama kwa watu wote, kuanzia ngazi ya zahanati mpaka hospitali ya Taifa.

Sambamba na hilo, amesema, Serikali ya Rais Dkt. Samia inaendelea kuhakikisha uboreshaji wa huduma kwa wananchi kwa kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa vifaa tiba, dawa pamoja na ujenzi wa miundombinu katika ngazi zote kuanzia taifa mpaka zahanati.