Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

CHMT MEATU KUVUNJWA KWA KUSHINDWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE

Posted on: April 4th, 2024


Mkurugenzi wa huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kuivunja Timu ya uendeshaji wa huduma za Afya ya Halmashauri (CHMT) ya Meatu baada ya kushinndwa kutekeleza majukumu yake.

Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo katika kikao cha majumuisho ya ziara ya kukagua shughuli za uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Afya katika mkoa wa Simiyu akiwa ameambatana na timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Akitoa ufafanuzi wa maelekezo hayo katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Mfaume amesema CHMT ya Meatu imeshindwa kufanya ufuatiliaji wa udhibiti wa mlipuko wa Kipindupindu uliopo katika eneo hilo, ufuatiliaji wa huduma za Afya pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya katika kituo cha Afya Mwandoya,Mwaisengela na Iramba ndogo.

“Hatujaja Simiyu kutafuta makosa lakini tunapoona mambo hayajaenda vizuri lazima tuseme na hili suala la kupambana na kipindupindu tumeona mkoa unapambana na isingekuwa kupambana hali isingekuwa hivi tunavyoiona lakini wengine wakipewa maelekezo ni shida hawafanyi mpaka timu itoke mkoani na kwea Meatu tumeona hali ni mbaya sana na hali tulioiona kwenye kituo cha Afya Mwandoya CHMT haijui kama kuna wagonjwa watano pale nikasema hawa wanaweza kufanya ufuatiliaji kwenye jamii ” amesema Dkt. Mfaume

Akisisitiza kuhusu utendaji usioridhisha wa CHMT hiyo, Mkurugenzi huyo amesema sema kwa mujibu wa kikao kilichofanyika kati ya timu kutoka TEMISEMI na Mkurugenzi wa Halmashauri kilionesha mkurugenzi wa halmashauri kuichoka timu hiyo.

Naye, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Prisca Kayombo ameahidi kufanyia kazi maelekezo hayo kwa kushughulika na watumishi wazembe na CHMT ya Meatu.

Timu ya Afya,Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI imelekea mkoa wa Mara na itakagua shughuli za uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Afya katika mkoa wa huo.