Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

CHALAMILA AWATAKA WANANCHI KUZINGATIA USHAURI WA WATAALAMU WA AFYA KUEPUKA MAGONJWA

Posted on: July 15th, 2023

Na. Mwandishi Wetu, Dar Es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Albert Chalamila amewataka wananchi kuzingatia ushauri wa afya unaotolewa na wataalamu ikiwemo kula kadri inavyoshauriwa na wataalamu ili kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo magonjwa ya Figo.

Mh. Chalamila alisema hayo wakati wa kuhitimishwa kwa mbio za Figo Marathoni zilizofanyika leo katika viwanja vya mnazi mmoja kwa lengo kukusanya fedha za kusaidia wahanga wa maradhi ya Figo ambazo zimeratibiwa na MNH kwa kushirikiana na taasisi ya Healthier Kidney Foundation

“Sisi tulio hai ndio tuna nafasi ya kusikiliza ushauri wa kitaalamu na kuufanyia kazi kwa mustakabali wa afya zetu, huwa nikimsikiliza Prof. Janabi anapotoa elimu naona kabisa vitu vingi anavyofundisha vinanigusa kabisa, ni nafasi ya kila mmoja wetu kupanga kubadilika sasa kwa kuwa tumeshasikia tatizo la Figo ni kubwa” alisema Mh. Chalamira

Aidha aliwataka wananchi kuwa na utaratibu wa kukata bima za afya ili ziweze kuwafaa pindi wanapopata maradhi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi aliwataka wananchi kuwekeza katika afya kama ambavyo wanawekeza kwa ajili ya kupata mafao ya uzeeni.

Alisema kuwa asilimia 90 hadi 95 ya wagonjwa wanaochuja damu (Dialysis) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (Upanga & Mloganzila) wamepata maradhi ya Figo kutokana na changamoto ya shinikizo la juu la damu.

“Tafiti zinaonesha kuwa katika wanaume watano basi mmoja ana shinikizo la juu la damu iwe ana jua au hajui, natoa wito kwa wananchi kuwa na utaratibu wa kufanya uchunguzi wa afya kila mwaka na wanapobainika kuwa na changamoto za shinikizo la juu la damu kutumia dawa kama inavyoshauriwa wa wataalamu” alisema Prof. Janabi

Naye, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Jonathan Mngumi alisema kuwa maradhi ya Figo yanaongezeka kila siku na kwamba asilimia 10 ya watu duniani sawa na watu milioni nane wanachangamoto za maradhi ya Figo.

“Katika Kliniki ya Kuchuja damu Muhimbili Upanga tunahudumia wagonjwa kati ya 90 hadi 120 wakati Mloganzila 30 hadi 50 kwa siku” alieleza

Dkt. Mngumi alitaja sababu zinazosababisha maradhi ya Figo kuwa ni matumizi holela ya dawa, shinikizo la juu la damu na kisukari pamoja na tabia bwete