Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

CANADA KUENDELEA KUCHANGIA MFUKO WA AFYA WA PAMOJA ILI TANZANIA KUFIKIA AFYA KWA WOTE

Posted on: May 16th, 2024



Na WAF - Dar Es Salaam

Serikalo ya Canada imeihakikishia Tanzania kuwa itaendelea kushirikiana pamoja katika kuboresha Sekta ya Afya ili kufikia malengo ya afya kwa wote huku huduma bora za afya zikiendelea kutolewa na kupatikana kwa uhakika.

Hayo yameelezwa Mei leo 16, 2024 kwenye kikao kilichowakutanisha Waziri wa Afya Mhe Ummy Mwalimu na Waziri wa Maendelo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussen katika Kikao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar Es Salaam.

"Fedha za Basket zimekuwa chanzo cha uhakika cha kugharamia huduma za afya kwenye vituo ngazi ya Zahanati hadi Hospitali za Wilaya. Zaidi ya hayo, utaratibu wa Ufadhili wa Moja kwa Moja wa Kituo cha Afya umeongeza uwajibikaji na uwazi kupitia ushirikishwaji zaidi wa jamii na ufuatiliaji wa utendaji wa matokeo ya afya ya vituo." Amesema Waziri Ummy

Pamoja na hilo, Waziri @ummymwalimu ameiomba Serikali ya Canada kusaidia na kushirikiana pamoja na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote na kusaidia uendelevu wake unafanikiwa. Hii ikijumuisha upatikanaji wa fedha pamoja na upatikanaji wa Bima kwa wananchi wote ikiwemo walio katika Sekta isiyo rasmi.

Aidha, Waziri Ummy amesema miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika mashirikiano baina ya Tanzania na Canada ni pamoja na kupungua kwa kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka Mitano kutoka asilimia 67 mwaka 2016 hadi asilimia 43 mwaka 2022 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai.

Kwa upande wake Waziri wa Waziri wa Maendelo ya Kimataifa wa Canada Mhe. Ahmed Hussen ameahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika Sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na kuendelea kuchangia katika mfuko wa Afya wa pamoja, afua za lishe, kuimarisha huduma za afya kabla ya uzazi na kuimarisha afya ya uzazi kwa wasichana na wanawake walio pembezoni.

Aidha, katika swala la Bima ya Afya kwa wote Mhe. Ahmed Hussen amesema katika nchi yao Serikali hugharamia matibabu kwa wananchi wote ambapo usimamizi wa huduma hizo hutumika kupitia Mfumo wa majimbo.