Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BODI MPYA MKEMIA MKUU WA SERIKALI YATAKIWA KUSIMAMIA UPELELEZI MASUALA YA JINAI

Posted on: February 20th, 2025

Na WAF - Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe ameitaka Bodi mpya ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kusimamia majukumu ya upelelezi wa masuala yanayohusu jinai ambayo yanaweza kuchangia na kuwezesha ufanisi katika mnyororo wa utoaji haki ndani na nje ya Serikali.

Dkt. Shekalaghe amesema hayo Februari 19, 2025 akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama kwenye uzinduzi wa Bodi hiyo ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali aliyoizundua katika jengo la Mkemia Mkuu, jijini Dar es Salaam.

"Bodi hii ina majukumu mengi, majukumu hayo ni pamoja na usimamizi wa kuwezesha upelelezi wa masuala yanayohusu jinai, masuala mbalimbali yanayohusiana na tiba, pamoja na kulinda usalama wa nchi, afya na mazingira dhidi kemikali hatarishi," amesema Dkt. Shekalaghe.

Aidha, Dkt. Shekalaghe amesema, pamoja na Bodi hiyo kuwa na jukumu la kusimamia utekelezaji wa masuala mbalimbali ya kisera yanayohusu mamlaka, majukumu yao mahususi yameainishwa katika kifungu cha 7 (1) na kifungu cha 8 cha Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na kanuni ya 3 ya kanuni za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali za mwaka 2017.

"Majukumu mahususi ya Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ni pamoja na kusimamia uendeshaji na utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kutengeneza miongozo na maelekezo yatakazowezesha utekelezaji wa Sheria ya Mamlaka," amesema Dkt. Shekalaghe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw. Christopher Kadio kwa niaba ya wajumbe wake, wameahidi kutekeleza maelekezo yote kwa vitendo yaliyotolewa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama kwa kuhakikisha wananchi wanapata haki zao.

"Sambamba na hilo, tutahakikisha kwamba bodi yetu inaanza kwa haraka kutatua changamoto zote zilizozoainishwa kwa kushirikiana taasisi nyingine za Serikali," amesema Bw. Kadio.