Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BMH YATOA MKONO WA EID KWA WAHITAJI

Posted on: April 10th, 2024


Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) imetoa Msaada wa chakula  kwa  Kituo cha Yatima cha Rahman cha Chang'ombe jijini Dodoma kama mkono wa Sikukuu ya Eid-el-Fitr.

Msaada huo umejumuisha mbuzi wawili, kilo 50 za mchele, kilo 50 za unga wa ngano pamoja na juisi na maji vimekabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Dkt Alphonce Chandika kwa Kituo hicho.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vyakula hivyo, Dkt Chandika, amesema BMH pamoja na kutoa huduma za afya, lakini wana wajibu wa kurudisha kwa jamii na kulea jamii inayowazunguka.

"Leo tumeona tuwakabidhi watoto yatima vyakula kama mkono wa Eid-el-Fitr ili waweze kusherehekea sikukuu kama watoto wengine," amesema Mkurugenzi Mtendaji, wakati akiongea na waandishi wa habari baada ya kukabidhi vyakula hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, aliambatana na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Hospitali, Prisca Lwangili, na Mwanasheria wa Hospitali, Advocate Alfred Kanan.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo, Rukia Hamis, ameshukuru kwa msaada huo, na  kusema, Hospitali hiyo imeonesha moyo wa Upendo kwa Wahitaji suala ambalo litawapatia thawabu kutoka kwa Mungu Mwenyewe.

"Tushukuru BMH kwa msaada huu lakini pia tuziomba taasisi nyingine ziige mfano wa BMH kwa kuwakumbuka watoto yatima nyakati za sikukuu ili watoto hawa waweze kufurahi sikukuu" amesema Rukia

Akisoma Historia ya  Kituo hicho, Bi Rukia amesema kituo kilianza 1998 kwa ajili ya kutatua changamoto za kinamama.

"Mwaka 2006, tukaona pia tutoe malezi kwa watoto wanaopitia changamoto hivyo tukaanza na watoto 15, Sasa hivi tuna watoto 150," anasema.