BILIONI 5.9 ZIMETUMIKA KUNUNUA VIUADUDU KATIKA HALMASHAURI NCHINI
Posted on: September 1st, 2023Na. WAF, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetumia kiasi cha shilingi Bilioni 5.9 kununua viuadudu katika ngazi ya Halmashauri ndani ya kipindi cha mwaka 2017 hadi 2023.
Hayo yaimebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel wakati akijibu maswali ya Wabunge katika kikao cha Bunge la 12.
Dkt. Mollel amesema ili kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa viuadudu kutoka kiwanda cha Kibaha kwa kipindi cha mwaka 2024-2026, Wizara ya Afya imeomba kupatiwa jumla ya Shilingi Bilioni 129.1 kwa ajili ya utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji wa viuadudu ili kuangamiza viluilui wa mbu kwenye mazalia ili kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo 2030.
“Wizara ya Afya inashirikiana na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Viwanda kuhakikisha Kiwanda kinapata ithibati kutoka Shirika la Afya Duniani ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza wa afua hii kutoka kwa wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria”. Ameeleza Dkt. Mollel.
Aidha, Dkt. Mollel amesema Serikali chini ya uongozi imra wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali zote ili kutatua changamoto ya dawa nchini.
Katika kutatua changamoto ya dawa nchini Dkt. Mollel amesema serikali imeanza utekelezaji wa kuipatia mtaji Bohari ya Dawa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ili kuwa na bidhaa za Afya muda wote.
Ameongeza kuwa Serikali imetoa fedha za ununuzi wa bidhaa za afya kila mwezi kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za Afya vya Umma ili kukabiliana na upungufu wa dawa.
Halikadhalika, Dkt. Mollel amesema Serikali itahakikisha suala la usimamizi wa bidhaa za afya linakuwa sehemu ya ajenda ya Kudumu ya Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa pamoja na kusimamia watoa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya ili kuweza kukadiria kwa usahihi (Forecasting).
“Vituo vya kutolea huduma za afya kutumia fedha zinazotokana na malipo ya huduma na dawa kununua bidhaa za afya kuliko kutegemea fedha zinazotolewa na Serikali pekee pia itasaidia kutatua changamoto ya upungufu wa dawa vituoni”. Amesema Dkt. Mollel.