Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BILIONI 21.1 KUNUNUA VIFAA TIBA KUBORESHA HUDUMA ZA UZAZI

Posted on: September 3rd, 2024

Na WAF - Dodoma, Bungeni


Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 21.1 kwa ajili ya kununua vifaa tiba vitakavyowezesha kuboresha huduma za uzazi kwa akina mama wakiwemo wenye ulemavu katika Mwaka wa fedha 2024/2025. 


Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amesema hayo leo Septemba 4, 2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Vitu Maalum Mhe. Stela Ikupa aliyetaka kujua ni Hospitali ngapi zimetenga vyumba vya kujifungulia wanawake wenye ulemavu nchini. 


Wakati akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Hospitali zote za Rufaa za Mikoa 28, Hospitali Sita za Kanda ambazo ni CCBRT, Mtwara, Chato Bugando, KCMC na META Mbeya zina vyumba vya kujifungulia ikiwemo wanawake wenye walemavu. 


"Lakini pia Hospitali zote 184 za Halmashauri zina vyumba vya kujifungulia wanawake wakiwemo wanawake wenye ulemavu na hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan." Amesema Dkt. Mollel