Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

BENKI YA DUNIA YAONESHA UTAYARI KATIKA AFUA ZA AFYA NCHINI TANZANIA

Posted on: December 21st, 2021

Na Atley Kuni, WAMJW, DSM

Benki ya Dunia imeonesha utayari kwa Tanzania katika uwekezaji wa kiwanda cha kuzalisha dawa za binadamu na kusaidia masuala ya Chanjo ya Uviko 19, Mama na Mtoto, ili kuwezesha wananchi  kupata dawa kwa wakati pindi wanapofuata huduma katika vituo vya kutoa huduma za Afya hapa nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya Dunia na Masuala ya Maendeleo ya Watu kwa Nchi za Tanzania, Zambia, Malawi na Zimbabwe Bw. Inaam Ui-Haq, amesema hayo leo 24 Disemba 2021 Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Dorothy Gwajima (Mb) ambapo amesema, kinachotakiwa Tanzania iwasilishe maombi ya uwekezaji ili kuwezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya kijamii.

“Benki ya Dunia, tupo tayari kusaidia Tanzania, lakini vema likapatikana Andiko juu ya Uviko -19, Pamoja na masuala ya Mama na Mtoto, kwa maeneo ambayo kama nchi inaona ni muhimu kuyaangazia kwa upekee” amesema  Inaam Ui-Haq, ambaye ni Mwakilishi wa Benki ya Dunia.

Akiongea katika Mazungumzo hayo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Dorothy Gwajima, amemhakikishia Mwakilishi wa Benki ya Dunia, kufikisha ujumbe wake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na kumweleza utayari wake katika kufikia azma ya kuwahudumia wananchi ili wajikinge na ugonjwa wa Uviko 19.

“Kwa sasa tupo katika awamu ya Pili ya Mpango Shirikishi na Harakishi kwenye Masuala ya kupambana na Covid -19, ambao tuliuzindua mkoani Arusha Kaskazini mwa nchi yetu Disemba 22, 2021, na maelekezo yamekwenda kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambao kwa Pamoja wanashirikiana kwa karibu zaidi na wananchi katika kutoa elimu ya chanjo kwa kuwatumia watoa huduma kwenye ngazi ya msingi kisha kupatiwa chanjo” amesema Mhe.Dkt. Gwajima 

Waziri Gwajima, amesema kuwa, Wizara ya Afya  wamefanya mpango wa kushirikisha jamii, viongozi wa Dini, watu maarufu na waandishi wa habari kwa lengo la kuwafikia watu wengi zaidi ili kufikia asilimia 60 ya wananchi watakaopatiwa chanjo 

MWISHO