BARAZA LA WAUGUZI KUWATUNUKU VYETI WAUGUZI NA WAKUNGA ZAIDI YA 1200.
Posted on: December 5th, 2021.Na Atley Kuni, WAMJW, DODOMA
Msajili wa Baraza la Wauguzi na Wakunga nchini, Bi. Agnes Mtawa, amesema wauguzi wapatao 1224, watatunukiwa vyeti mbalimbali ikiwa ni hatua ya kuwatambua wauguzi/wakunga hao na sifa zao mara baada ya kufaulu mitihani ya baraza hilo, iliyofanyika mapema mwezi Agosti, 2021.
Akizungumza na wandishi wa Habari jijini hapa, Bibi Mtawa alisema, baraza hilo huwatambua wauguzi na wakunga hao mara baada kufanya na kufaulu mitihani ya bodi na kisha kusajiliwa kulingana na viwango vyao vya elimu kuanzia ngazi ya Stashada, Astashahada Pamoja na Shahada.
“Tunategemea kuwa na mahafali tarehe 08. Desemba, 2021, ambapo jumla ya wauguzi na wakunga 1224, waliosajiliwa kwa Shahada (29), Astashada (1096), Stashada (99), wataapishwa na kupewa vyeti vya usajili na leseni ambazo watatumia wakati wote wa kutoa huduma” amesema Mtawa na kuongeza kuwa, katika zoezi hilo “Watakula kiapo cha utiifu na maadili kutoa huduma bora kwa wananchi, amesisitiza msajili huyo wa Baraza.
Bi.Mtawa amewakumbusha wauguzi na wakunga kuhakikisha popote watakapokuwa kuhakikisha wanajisomea ili kuwa na elimu endelevu ili kudumisha weledi wao na kwenda sambamba na mabadiliko mbalimbali ya teknolojia kwani hili ni takwa la kisheria ambalo ni lazima lifanyike kila baada ya miaka mitatu.
Bi.Mtawa, ameendelea kuwakumbusha mambo saba yanayo ongoza taaluma hiyo ikiwepo kuheshimu utu wa mtu na uhai, kuomba ruhusa kabla ya kutoa huduma kwa mteha, kudumisha weledi wa kitaaluma, kuwajibika na uwajibikaji kwa lolote utakalolifanya kuwa mwaminifu na kuzingatia usawa, kushirikiana na watendaji wengine kama sehemu ya timu Pamoja na kulinda siri ya wateja.
Baraza linajukumu la kuonya, kukaripia, kuamuru usimamishwaji wa kutoa huduma, au kuamuru kuondolewa au urejeshwaji katika Rejista au Orodha jina la muuguzi au mkunga yeyote aliyesajiliwa au kuorodheshwa kutokana na makosa ya kiutendaji, uzembe au makosa ya kitaaluma.
MWISHO