Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ASILIMIA 92 YA WASICHANA WENYE UMRI WA MIAKA 14 WAMEPATA CHANJO YA HPV

Posted on: May 14th, 2024

UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA YA AFYA 2023/24Na WAF - Dodoma

Serikali imeendelea kuwalinda wasichana wenye umri wa miaka 14 dhidi ya Saratani ya mlango wa kizazi kwa kununua na kusambaza chanjo ya Human Papilloma Virusi (HPV) kulingana na mahitaji ya chanjo hiyo hapa nchini.

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema hayo Bungeni Mei 13, 2024 akiwa anawasilisha hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 akielezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika utoaji wa huduma za Kinga nchini.

“Hadi kufikia mwezi Machi 2024 jumla wasichana 663,949 walikuwa wamepatiwa chanjo ya HPV sawa na asilimia 92 ya walengwa ikilinganishwa na Wasichana 535,708 waliopata chanjo hiyo kwa kipindi kama hicho mwaka 2022/2023.” Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy Mwalimu amesema lengo lilikuwa ni kuchanja jumla ya wasichana laki 721,684 wenye umri wa miaka 14 kwa ajili ya chanjo ya HPV ili kuwakinga wasichana hao dhidi ya Saratani ya mlango wa kizazi.

“Chanjo ni moja ya njia zilizothibitika kisayansi kuzuia magonjwa, hivyo nichukue fursa hii kuwahimiza wananchi hususan wazazi/walezi wenye watoto wa umri chini ya miaka mitano (5) kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yanayozuilika na chanjo kama inavyoshauriwa na wataalam wa afya.” Amesema Waziri Ummy