Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ASILIMIA 81 YA WAJAWAZITO WANAJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA KUTOA HUDUMA ZA AFYA

Posted on: December 18th, 2023

Na. WAF - Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema asilimia 81 ya wajawazito nchini wanajifungulia katika vituo vya kutoa huduma za Afya ukilinganisha na asilimia 63 kwa mwaka 2016.

Waziri Ummy amesema hayo leo Disemba 18, 2023 kwenye ukurasa wake wa X wakati akifafanua juu ya upotoshaji unaondelea katika mitandao ya kijamii kuhusu wajawazito kujifungulia chini. 

“Ukweli utabaki kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza sana katika kuboresha huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ambapo kwa sasa asilimia 81 ya wajawazito nchini wanajifungulia katika vituo vya kutoa huduma za Afya.” Amesema Waziri Ummy 

Aidha Waziri Ummy amesema vifo vya wajawazito vimepungua kutoka vifo 556 katika kila vizazi hai laki 100,000 hadi vifo 104 katika kila vizazi hai laki 100,000, Namba zinaongea.

Akiendelea kufafanua malalamiko hayo Waziri Ummy amesema katika Sekta ya Afya kila siku zinaibuka changamoto mpya hivyo haiwezekani kumaliza changamoto zote kwa siku moja au muhula mmoja. 

“Tutaendelea kuchukua hatua mahususi ili kuzitatua kwa haraka changamoto za utoaji huduma za Afya nchini kadri zinavyojitokeza Serikali ya Rais Samia inazipa kipaumbele cha hali ya juu huduma za Afya ya Uzazi, mama na mtoto.