Customer Feedback Centre

Ministry of Health

ASANTENI MADAKTARI BINGWA WA SAMIA KUTUFIKIA MWANZA - RC MTANDA

Posted on: June 17th, 2024


Na WAF - MWANZA


Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, amewapokea jumla ya Madaktari Bingwa 45 na kuwashukuru kwa kuwafikia huku akiahidi kuwapa ushirikiano kwa kipindi chote cha siku tano watakapokua mkoani humo.


Akitoa Salaam za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana, amesema wananchi walio wengi wana changamoto na uhitaji wa huduma za kibingwa lakini wanashindwa kuzipata kutokana na gharama.


"Mkoa wa Mwanza ambao una wananchi wasiopungua milioni nne kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, ni wazi kwamba huduma hii ya Kibingwa na Ubingwa Bobezi ni Muhimu kwetu". Amesema Balandya.


Katibu Tawala huyo amewaelekeza Madaktari wa Hospitali za Wilaya kuwapa ushirikiano Madaktari hao Bingwa kwa siku zote watakazo kuwepo mkoani hapo.


"Wataalam hawa watakuwa kwenye wilaya zetu zote nane na Halmashauri ya Ukerewe watakuwa na vituo viwili, ni rai yangu kwa wananchi kutumia fursa hii tukapime afya zetu". Amehimiza Balandya.


Awali akitoa Salaam za Wizara ya afya Afisa Progamu uzazi salama Fidea Obimbo, amesema huduma hiyo ya kibingwa tayari imefika kwenye Halmashauri 138 na Mikoa 20 mpaka sasa.


"Tangu kuzinduliwa kwa mpango huu wananchi zaidi ya 50,000 wamefikiwa na huduma za kibingwa, ikiwepo wanachi 3,641 waliofanyiwa huduma za upasuaji kutikana na changamoto kadhaa za afya." Amesema Bi. Obimbo


Madaktari Bingwa hao, watakuwa wa Usingizi na Ganzi, Watoto, Wanawake, Magonjwa ya Ndani, Upasuaji na kwa Halmashauri ya Buchosa atakuwepo pia Bingwa Macho.