Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

ARUSHA YAJADILIWA KUWA KITOVU CHA TIBA UTALII

Posted on: September 26th, 2024

Na. WAF, Arusha

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Bw. Ismail Rumatila, amekutana na kujadiliana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, juu ya mikakati ya sekta ya afya na mipango ya kuifanya Arusha kuwa kitovu cha tiba utalii nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo, Septemba 26, 2024, mara baada ya Naibu Katibu Mkuu kumaliza ziara yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, ambapo amepata fursa ya kutathmini huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo na kuwapongeza watumishi kwa jitihada zao za kuboresha huduma za afya.

Katika ziara hiyo, Bw. Rumatila ameelezea kuridhishwa kwake na huduma bora zinazotolewa katika Hospitali ya Mount Meru, akibainisha kuwa hospitali hiyo ni mfano mzuri wa utoaji huduma bora kwa wananchi wa Arusha na wageni wanaotembelea mkoa huo.

Aidha, amesema kuwa kutokana na Jiji la Arusha kuwa kitovu cha utalii wa kimataifa ina nafasi kubwa ya kuwa kitovu cha tiba utalii hasa kwa kuzingatia mikusanyiko ya watu kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja kwa ajili ya vivutio vya utalii.

“Arusha ni jiji la kimataifa lenye wageni kutoka mataifa mbalimbali, hasa kutokana na utalii wa mbuga za wanyama na michezo ya asili. Tunapozungumzia utalii wa tiba, tunaweza kuongeza vivutio kwa watalii hawa kwa kuwapatia huduma za matibabu ya hali ya juu sambamba na vivutio vya kawaida vya utalii,” amesema Bw. Rumatila.

Pia, amebainisha kuwa tiba utalii ni sekta inayokua kwa kasi duniani kote, na Tanzania, hivyo jiji la Arusha, lina fursa nzuri ya kuwekeza katika sekta hii kutokana na umaarufu wake wa utalii wa asili na urahisi wa kufikika kutoka mataifa mbalimbali.

Kwa upande wake, Mhe. Paul Makonda ameelezea shauku yake ya kuiona Arusha ikiimarisha sekta ya tiba utalii, akitoa wito kwa Wizara ya Afya kuwekeza zaidi katika miundombinu na huduma za afya ambazo zitavutia wageni kutoka nje kuja kupata matibabu nchini.

“Tunataka Arusha iwe kitovu cha tiba utalii, siyo tu kwa Tanzania, bali kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Hii itasaidia kuvutia zaidi wageni kutoka mataifa mbalimbali, siyo kwa ajili ya utalii wa wanyamapori pekee, bali pia kwa huduma za afya,” amesema Makonda.