Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

AFUA ZA KIFUA KIKUU, UKIMWI, MALARIA, HOMA YA INI, MAGONJWA YA NGONO NA UKOMA, KUPEWA KIPAUMBELE

Posted on: August 14th, 2024



Na WAF – Dar es Salaam

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya imeadhimia kuendelea kuzipa kipaumbele afua za Kifua Kikuu, UKIMWI, Malaria, Homa ya Ini, Magonjwa ya Ngono na Ukoma ili kukabiliana na maradhi hayo.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume Agosti 14, 2024 wakati wa mkutano wa mapitio ya programu za nusu mwaka kwa Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na homa ya Ini (NASHCOP), Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), na Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma (NTLP), jijini Dar es Salaam.


“Tumepiga hatua kubwa ya kupambana na Malaria, kupitia juhudi za kuongeza hafua za kinga na tiba zenye gharama nafuu, hatari ya malaria miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano imepungua hadi chini ya asilimia 10 tangu mwaka 2017, aidha, tumeona kupungua kwa idadi ya wagonjwa wa malaria kwa asilimia 70 katika vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huu,” amesema Dkt. Mfaume.



“Tanzania ni moja ya nchi 30 zenye wagonjwa wengi wa Kifua Kikuu, ikiwa na makadirio ya kiwango cha maambukizi ya kifua kikuu ya 195 kwa kila watu 100,000 na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU cha asilimia 16.4 miongoni mwa watu wenye kifua kikuu. Licha ya changamoto hizi, tumepiga hatua kubwa. Kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, tumegundua na kutibu zaidi ya wagonjwa wa kifua kikuu 431,000 wakiwemo watu wazima na takribani watoto 67,000. kifua kikuu sugu dhidi ya dawa inabakia kuwa tishio kubwa kwa afya ya umma, ambalo linahitaji umakini wa haraka na endelevu,” amesema Dkt. Mfaume.



Kwa upande wake, Mkuu wa Programu kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Catherine Joachim, alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya VVU. Utafiti wa Athari za VVU, Tanzania 2022-2023 unaonyesha kuwa asilimia 82.7 ya watu wanaoishi na VVU wanatambua hali zao, ambapo asil8mia 97.9 yao wanatumia dawa za kufubaza virusi vya VVU, na 94.3% wamepata udhibiti wa virusi.



Kwa upande mwingine, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani, (WHO) Dkt. Catherine Gitige, amesema Shirika hilo linaipongeza Tanzania kwa jitihada zake za kudhibiti UKIMWI pamoja na kuongeza wigo wa vyanzo endelevu vya kuhakikisha malengo ya kudhibiti ugonjwa huo yanafikiwa ifikapo mwaka 2030.