Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

DKT. SHEKALAGHE ATEMBELEA KIWANDA CHA ARVs KUANGALIA UTAYARI WA KUANZA UZALISHAJI

Posted on: December 1st, 2025

Na WAF, Arusha



Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe ametembelea kiwanda cha kuzalisha dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited  (TPI) kilichopo jijini Arusha kwa lengo la kujionea utayari wa kiwanda hicho kuanza kufanya kazi baada ya kusitisha uzalishaji kwa muda.


Akiwa katika kiwanda hicho leo Desemba Mosi, 2025 jijini Arusha, ambacho awali kilikuwa kinazalisha dawa , Dkt. Shekalaghe amesema hatua hiyo inatotokana na maelekezo ya Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa ya kutaka kiwanda hicho kufufuliwa ili kuendelea kuboresha upatikanaji wa dawa za ARVs, kuongeza ajira kwa wananchi na kuongeza pato la Taifa.


“Kiwanda hicho kinatakiwa kufufuliwa ili kuanza kuzalisha dawa kwani kiwanda hicho kimesimama kwa muda mrefu, hivyo nimeelekezwa na Waziri Mhe. Mchengerwa kuja kuona hatua za kuchukua kufufua na kuanza uzalishaji,” amesema Dkt. Shekalaghe.


Amesema Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa na Msajili wa Hazina wameingia ubia na TPI, ambao tayari umeshasainiwa na tayari uko kwenye taratibu ya kufufua kiwanda hicho.


“Baada ya kukaa na wataalam tumekubaliana kuunda timu ya wajumbe wa bodi na menejimeti itakayosimamia kazi hii ambayo kwa sasa imefikia asilimia 90 ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wataalam wanakagua ubora wa mitambo iliyopo," amefafanua Dkt. Shekalaghe.


Ameongeza kuwa mtazamo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kufufua viwanda ndani ya nchi na kuwakaribisha wadau kuwekeza katika viwanda hususani viwanda vya Afya ili  kuzalisha dawa wenyewe na  kupunguza gharama kwa Taifa pamoja na kusaidia kupatikana kwa dawa na vifaa tiba kwa haraka.