Maoni Ya Wateja

Wizara Ya Afya

SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA HUDUMA NA TAARIFA ZA AFYA YA MACHO

Posted on: November 29th, 2025

Na WAF, Morogoro

Serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu huduma za afya ya macho nchini, ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo Novemba 27, 2025 na Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiombukiza, kutoka Wizara ya Afya Dkt. Omary Ubuguyu, wakati akifungua kikao kazi cha waratibu wa macho wa mikoa nchini, mkoani Dodoma.

Dkt. Ubuguyu amesema kuwa, pamoja na kuwepo kwa miundombinu, vifaa na vifaa tiba, bado kuna umuhimu mkubwa wa kusimamia ubora wa huduma za afya ya macho ili kuhakikisha jamii inapata manufaa ipasavyo.

“Wizara itaendelea kuwafikia wananchi wenye matatizo ya macho ili kupunguza athari za uoni, hasa katika maeneo yenye changamoto kubwa za upatikanaji wa huduma,” amesema Dkt. Ubuguyu.

Aidha, Dkt. Ubuguyu ameweka wazi kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau ni msingi muhimu wa kuboresha huduma na kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma.

Dkt. Ubuguyu amebainisha kuwa baadhi ya mikoa bado ina upungufu wa wadau au ina idadi ndogo ya taasisi zinazotoa huduma za macho. Changamoto hiyo inahitaji jitihada za pamoja ili kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Macho kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Greater Mande, ameeleza kuwa upatikanaji wa huduma katika ngazi ya msingi umeendelea kuimarika kwa kiasi kikubwa, jambo linalowawezesha wananchi kupata huduma muhimu kwa urahisi na kwa wakati.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mikakati ya kitaifa utakuwa na mafanikio zaidi endapo kila mkoa utawasilisha taarifa kwa wakati na kufanya kazi kwa ukaribu na wadau wote walipo. Kwa kufanya hivyo, uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa huduma za macho utaongezeka na upatikanaji wa huduma bora nchini utaimarika.