TANZANIA INA DAWA ZA KUTOSHA ZA KUFUBAZA VIRUSI ZA UKIMWI
Posted on: December 2nd, 2025Na WAF, Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa licha ya kupata changamoto iliyotokana na baadhi ya wafadhili wa nje nchi kujitoa katika utekelezaji wa afua mbalimbali za kudhibiti maambukizi ya UKIMWI ikiwemo upatikanaji wa dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI, bado Tanzania ina dawa za kutosha hadi Oktoba 2026.
Hayo yamesemwa leo Desemba 1, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. William Lukuvi wakati akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari katika kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani.
Mhe. Lukuvi amesema maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani mwaka huu 2025 hayajafanyika kitaifa katika mkoa wowote ili fedha zilizotengwa kwenye bajeti pamoja na wadau mbalimbali zitumike katika kutekeleza afua za mapambano ya UKIMWI.
“Pamoja na Mataifa wafadhili kujitoa na kupunguza upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, Serikali imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI zinaendelea kupatikana nchi nzima na kutolewa bure kwa WAVIU katika vituo vya kutolea huduma za afya,” amesema Mhe. Lukuvi.
Aidha, Waziri Lukuvi ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuboresha afua mbalimbali za kudhibiti maambukizi ya VVU/UKIMWI ikiwemo elimu na afua za kinga, kuhamasisha wananchi kupima na kutambua hali zao za maambukizi, kutoa ushauri, upimaji, matunzo na huduma za dawa kwa wenye maambukizi.
Naye, Naibu Waziri wa afya Mhe. Florence Samizi amesema licha ya changamoto ya kupungua kwa wafadhili wa nje katika kutoa rasilimali za mapambano dhidi ya UKIMWI, Serikali kupitia vyanzo vyake vya ndani imetoa Shilingi Bilioni 189 katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vitendanishi na usafirishaji wa sampuli za maabara.
“Kiasi hiki cha fedha kimechangia kufanya hali ya upatikanaji wa ARVs kuwa asilimia 100 ambapo hakuna mteja aliyefika kituo cha kutolea huduma za afya na kukosa dawa,” amesema Naibu Waziri Samizi.
Dkt. Samizi ameongeza kuwa dawa zilizopo kwa sasa na zile zinazotegemewa kupokelewa ndani ya miezi sita ijayo, zitatosheleza matumizi hadi Oktoba 2026.