Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA YAKABIDHI MWONGOZO MPYA 2026 WA UONGEZAJI VIRUTUBISHI KWENYE CHAKULA

Posted on: August 14th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Dodoma

Wizara ya Afya imeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Uongezaji wa Virutubishi kwenye Chakula wa mwaka 2026 pamoja na Kanuni za Uongezaji wa Virutubishi kwenye Chakula za mwaka 2024, zinazotoa msingi wa kisheria na kiutendaji kwa wasindikaji kuzingatia taratibu na viwango vinavyotakiwa.

Hayo yamesema na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Eliud Eliakim, leo Agosti 13, 2026 jijini Dodoma wakati wa Hafla ya kukabidhi virutubishi vya Vitamini A na Mwongozo wa Uongezaji Virutubishi kwenye chakula wa mwaka 2026 kwa Chama cha Wasindikaji wa Maduta ya Alizeti Tanzania ( TASUPA), akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe

Amesema Wizara imekamilisha Mfumo wa Usimamizi na Ufuatiliaji wa Uongezaji wa Virutubishi kwenye Chakula na kununua na kusambaza mashine 12 za i-check kwa ajili ya kupima kiwango cha madini chuma kwenye unga wa ngano na mahindi katika mikoa 12 huku ikiwezesha upatikanaji wa Rapid Test Kits kwa ajili ya kupima madini joto kwenye chumvi, madini chuma kwenye unga na Vitamini A kwenye mafuta ya kula yaliyosafishwa.

Dkt. Eliud ameeleza kuwa Wizara pia imenunua lita 100 za Vitamin A Premix ambazo zinakabidhiwa kwa Chama cha Wasindikaji wa Mafuta ya Alizeti (TASUPA) kwa ajili ya kusambazwa kwa wasindikaji wadogo.

“Vilevile, Wizara imenunua na kusambaza Dosifier 160 katika mikoa 10 kwa ajili ya kusaidia wasindikaji wadogo kuongeza virutubishi kwenye unga, pamoja na mashine nne za kusafisha mafuta na kuongeza Vitamini A zinazofungwa katika vituo vya kusafishia mafuta vya Dodoma, Singida na Mbeya,” amesema Dkt. Eliud

Dkt. Eliud amesema kuwa Mwongozo huo utasaidia kuhakikisha vyakula vinavyotakiwa kuongezwa virutubishi, ikiwemo unga wa ngano, unga wa mahindi, chumvi na mafuta ya kula yaliyosafishwa, vinakuwa bora na salama kwa walaji.

Aidha, amesisitiza matumizi ya mkakati wa uongezaji wa virutubishi kwenye vyakula vinavyosindikwa kama njia muhimu ya kuongeza vitamin na madini katika chakula na kukabiliana na athari za upungufu wa virutubishi hivyo mwilini.