Wizara Ya Afya

TANZANIA YABAINISHA MAFANIKIO YA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI AFRIKA

Posted on: August 14th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Tanzania imeendelea kupata mafanikio katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa urahisi.

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo, Agosti 14, 2026, wakati akimwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, katika kikao kwa njia ya mtandao yenye kaulimbiu “The Unfinished Agenda: Confronting Africa’s Maternal, Newborn, Child and Adolescent Mortality Crisis” iliyoandaliwa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC), ambapo alishiriki akiwa jijini Dodoma.

Amesema mafanikio hayo yanatokana na jitihada mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali katika kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, ikiwemo kuwekeza katika miundombinu, wataalamu na upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi.

Aidha, Dkt. Samizi amesema hatua hizo zinaendelea kusimamiwa kwa uongozi wa kisiasa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuweka kipaumbele katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, hususan wanawake, wajawazito na watoto.

“Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeendelea kuwa chachu ya maboresho katika sekta ya afya, kwa msisitizo mkubwa katika kuhakikisha kila mama na mtoto anapata huduma kwa wakati na kwa ubora unaostahili,” amesema Dkt. Samizi.

Ameeleza kuwa Serikali pia imeendelea kupunguza changamoto ya umbali wa wananchi kufuata huduma za afya kwa kusogeza huduma karibu na jamii, ikiwemo lengo la kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana ndani ya umbali wa kilomita tano.

Dkt. Samizi amesema ushawishi na uongozi wa kisiasa katika kuhamasisha wanawake kutumia huduma za afya mapema, hususan kuhudhuria kliniki mara tu wanapobaini ujauzito, ni miongoni mwa hatua zinazochangia kuimarisha usalama wa mama na mtoto.