SERIKALI NA WADAU WAIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA, WAGONJWA MAHUTUTI NA WATOTO
Posted on: August 14th, 2026Na Zakayo Mosha – WAF
Ruvuma
Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI pamoja na Mdau wa Maendeleo Clinton Health Access Initiative (CHAI), imeendelea kutekeleza afua mbalimbali za kuimarisha maandalizi na utoaji wa huduma za dharura, matibabu kwa wagonjwa mahututi na watoto wachanga nchini.
Hayo yamesemwa leo, Agosti 14, 2026, mkoani Ruvuma na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura kutoka Wizara ya Afya Dkt. Michael Kiremeji, wakati akihitimisha zoezi la ufuatiliaji wa mafunzo kwa vitendo lililofanyika Agosti 10 hadi 14, 2026 katika mikoa ya Arusha, Manyara, Morogoro, Dodoma, Mbeya, Pwani, Mwanza, Mtwara na Ruvuma.
"Zoezi hili limefanyika kwa ufanisi mkubwa katika vituo vya afya na mikoa yote iliyokusudiwa, likiwahusisha wataalam kutoka Wizara ya Afya, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya pamoja na vituo husika," amesema Dkt. Kiremeji
Ameongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, wataalam wa afya wanaohudumu katika vitengo vya dharura wamejengewa uwezo na kuongezewa ujuzi na maarifa ya namna bora ya kutoa huduma muhimu za dharura kwa wagonjwa mahututi na watoto wachanga.
“Uboreshaji wa utoaji wa huduma za dharura katika Hospitali za Wilaya na Mikoa hapa nchini umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo, pamoja na kupunguza gharama kwa wagonjwa na ndugu zao za kufuata huduma hizo katika maeneo ya mbali na wanapoishi,” amesema Dkt. Kiremeji
Kwa upande wake, Afisa Programu wa Mradi wa Upatikanaji wa Hewa Tiba ya Oksijeni kutoka CHAI, Bi. Happy Ndomba amesema, CHAI itaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia Idara ya Dharura na Maafa katika kuboresha utoaji wa huduma za dharura kwa wagonjwa mahututi na watoto wachanga, hususan watoto njiti na wale wanaohitaji msaada wa hewa tiba mara baada ya kuzaliwa.
Aidha, Bi. Ndomba amesema CHAI itaendelea kusaidia utoaji wa mafunzo kwa vitendo kwa wataalam wa afya katika Hospitali za Wilaya na Mikoa, pamoja na kusaidia katika uboreshaji wa miundombinu na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.
Dkt. Kiremeji ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa ushirikiano mzuri na CHAI katika kuimarisha utoaji wa huduma muhimu.