UWEKEZAJI KATIKA TAFITI, ELIMU WAONGEZA UWEZO KUBAINI MAGONJWA ADIMU
Posted on: August 14th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amesema Serikali imeendelea kuongeza uwekezaji katika tafiti, teknolojia na elimu ya afya, hatua iliyosaidia kuongeza uwezo wa nchi kubaini na kuelewa magonjwa adimu pamoja na kuweka mikakati madhubuti ya kuwahudumia wananchi wanaoishi na changamoto hizo.
Dkt. Magembe amesema hayo leo Agosti 13, 2026, alipokuwa akijibu maswali ya Wabunge katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, baada ya kuwasilishwa taarifa kuhusu hali na athari za magonjwa adimu katika Kumbi za Bunge, Mkoani Dodoma.
Amesema uwekezaji huo umewezesha kuongeza idadi ya maabara zinazofanya uchunguzi wa genomic kutoka maabara moja hadi sita, jambo lililoongeza uwezo wa kufanya uchunguzi, utambuzi na tafiti zinazohusiana na magonjwa adimu.
Aidha, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu magonjwa adimu ambayo itaendelea kutolewa kupitia watoa huduma ngazi ya jamii, watumishi wa afya pamoja na vyombo vya habari ili kuongeza uelewa na kuchochea hatua stahiki za kiafya.
Dkt. Magembe amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji katika maabara za genomic, tafiti, elimu kwa jamii na rasilimali fedha ili kuongeza uwezo wa kubaini magonjwa adimu na kupanga huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.