SERIKALI YAONGEZA NGUVU KUDHIBITI MAGONJWA ADIMU NCHINI
Posted on: August 14th, 2026Na Hassan Kimweri, WAF – Dodoma
Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa watu wanaoishi na magonjwa adimu kwa kuboresha utambuzi wa magonjwa hayo, upatikanaji wa dawa na matibabu pamoja na kuongeza uwezo wa wataalamu wa afya ili huduma kupatikana kwa wakati na kwa kuzingatia misingi ya Afya kwa Wote.
Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema hayo leo Agost 13, 2026 wakati akiwasilisha taarifa ya athari za magonjwa adimu mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI katika kumbi za Bunge Mkoani Dodoma.
Dkt. Samizi amempongeza na Kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika mapambano dhidi ya magonjwa haya kwa kutenga fedha ili kufanya ugunduzi, uchunguzi na kusomesha mabingwa wa ubingwa na ubobezi ili kusaidia huduma hizo kutolewa hadi katika ngazi za chini kwa baadae.
"Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa adimu ni hali ya kiafya inayomwathiri chini ya mtu mmoja kati ya watu 2,000, huku duniani kukiwa na zaidi ya magonjwa adimu 7,000 yanayoathiri zaidi ya watu milioni 300," amesema Dkt. Samizi
Aidha, Dkt. Samizi amesema Nchini Tanzania, magonjwa hayo yanakadiriwa kuwaathiri watu milioni moja hadi milioni tatu yakiwemo ya Sikoseli, Himofilia, baadhi ya magonjwa ya kinga ya mwili na magonjwa yanayoathiri mfumo wa fahamu na misuli.
"Tanzania inakadiriwa kuwa na watoto takribani milioni 14,000 wanaozaliwa na Sikoseli kila mwaka, huku asilimia 15 hadi 20 ya Watanzania wakiwa na vinasaba vya ugonjwa huo, hatua inayoonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma za ugonjwa huo," amesema Dkt. Samizi
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Dkt. Samizi amesema Serikali imeboresha mifumo ya taarifa kupitia DHIS2 na GhoTHOMIS ili kuimarisha ukusanyaji na ufuatiliaji wa takwimu za wagonjwa, sambamba na kuhimiza tafiti kuhusu magonjwa adimu pamoja na huduma za utengamao, tiba shufaa na msaada wa kisaikolojia.
Mwisho, Dkt. Samizi amesema magonjwa adimu yanaweza kusababisha athari kubwa kiafya, kijamii na kiuchumi kutokana na kuchelewa kutambuliwa, gharama kubwa za matibabu, upungufu wa wataalamu