Wizara Ya Afya

JKCI, CCBRT ZANUFAIKA NA MILIONI 200 KUPITIA MBIO ZA HISANI ZA CRDB

Posted on: August 16th, 2026

Na Shaban Juma, WAF – Dar es Salaam

Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na CCBRT imepokea jumla ya Shilingi milioni 200, ambapo kila taasisi imepatiwa Shilingi milioni 100, ikiwa ni sehemu ya fedha zilizopatikana kupitia mbio za hisani zilizoandaliwa na CRDB Bank Jijini Dar es Salaam.

Mbio hizo zimefanyika leo Agosti 16, 2026 Jijini Dar es Salaam, zikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kushiriki katika michezo na mazoezi ya mwili kwa ajili ya kuimarisha afya, huku fedha zitokanazo na mbio hizo zikielekezwa katika kusaidia huduma za afya na makundi mbalimbali yenye uhitaji.

Mbio hizo zimejumuisha kilomita tano (5), kilomita 10, kilomita 21, kilomita 42 pamoja na mbio maalum za baiskeli za kilomita 65, na kushirikisha wananchi kutoka makundi mbalimbali.

Katika tukio hilo, Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi, akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, wameshiriki katika mazoezi na mbio hizo, ambazo Mgeni Rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.

Tangu kuanza kwa mbio hizo za hisani, zaidi ya watoto 400 pamoja na kina mama 240 wamenufaika na huduma mbalimbali za matibabu, ikiwa ni sehemu ya mchango wa mbio hizo katika kuunga mkono upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Fedha hizo Shilingi milioni 200 zilizotolewa kwa JKCI na CCBRT zitaendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha huduma za afya, ikiwemo mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo na saratani pamoja na kuboresha huduma kwa mama na mtoto.

Mbio hizo pia zimeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi mara kwa mara, kuzingatia lishe bora na kuchukua hatua za mapema katika kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Ushiriki wa Wizara ya Afya katika mbio hizo unaendana na juhudi za Serikali za kuimarisha afya kinga na kuhamasisha jamii kuchukua hatua katika kulinda afya zao, huku ushirikiano na wadau wa sekta binafsi ukiendelea kuongeza nguvu katika utoaji wa huduma za afya nchini.