Wizara Ya Afya

WIZARA YA AFYA, UNICEF KAZINI KUIANDAA JAMII KUKABILIANA NA EL NIÑO NA EBOLA SHINYANGA

Posted on: September 23rd, 2026

Na WAF – SHINYANGA

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) imeanza ziara ya uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utayari wa wananchi kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola (EVD) pamoja na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino.

Akizungumza leo Septemba 23,2026 Mkoani Shinyanya, wakati wa kikao kazi cha uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii kilichofanyika katika Manispaa ya Shinyanga, Afisa kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Bw. Penford Wangeleja, amesema maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha jamii inaelewa hatari zinazoweza kujitokeza na namna ya kuchukua hatua stahiki mapema.

Bw. Wangeleja amesema ushiriki wa jamii ni sehemu muhimu katika kukabiliana na majanga na magonjwa ya mlipuko, hivyo, wananchi wanapaswa kuwa na uelewa wa namna ya kujikinga, kutoa taarifa mapema na kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka za afya.

“Tunataka jamii iwe sehemu ya maandalizi haya, kwa sababu utayari dhidi ya Ebola na majanga yanayoweza kutokana na El Niño hauwezi kufanikiwa bila ushiriki wa wananchi wenyewe, ni muhimu wananchi kufahamu hatua za kuchukua, kutambua viashiria vya hatari na kufuatilia taarifa rasmi,” amesema Bw. Wangeleja.

Amesema ziara hiyo pia inalenga kuimarisha mifumo ya tahadhari na mwitikio wa haraka, sambamba na kuongeza uwezo wa timu za afya katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri katika kutoa elimu na kukabiliana na dharura zinazoweza kuathiri afya ya jamii.

Kwa mujibu wa Bw. Wangeleja, mwingiliano mkubwa wa kibiashara wa Shinyanga na maeneo ya nchi jirani pamoja na shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika mkoani humo ni miongoni mwa mambo yanayohitaji kuzingatiwa katika kuimarisha utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola.

Amesema kwa upande wa mvua za El Niño zinazotarajiwa kunyesha, jamii inapaswa kuchukua hatua za mapema kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo kushiriki katika usafi wa mazingira, kuzibua mitaro na kuhakikisha maeneo ya makazi yana njia salama