Wizara Ya Afya

MHE. MCHENGERWA AAGIZA TAARIFA ZA BIMA YA AFYA KWA WOTE KUWASILISHWA KWA WAKATI

Posted on: October 12th, 2026

Na Hassan Kimweri, WAF - Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amewaelekeza viongozi wa mikoa na halmashauri kuimarisha utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha Serikali kufuatilia maendeleo ya mpango huo, kubaini changamoto na kuchukua hatua za kuzitatua kwa wakati.

Ametoa maelekezo hayo leo Oktoba 12, 2026 wakati wa kikao kazi chake na Wakuu wa Mikoa kuhusu ajenda ya Bima ya Afya kwa wote, kilichofanyika jijini Dar es Salaam

Amesema katika siku 14 za mwanzo za utekelezaji, taarifa zinapaswa kuwasilishwa kila siku jioni, na baada ya kipindi hicho taarifa za kila wiki ziwasilishwe kila Jumatatu asubuhi kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Ameeleza kuwa taarifa hizo zinapaswa kuonesha idadi ya kaya zilizosajiliwa na kukamilisha masharti ikilinganishwa na malengo yaliyowekwa, utayari wa vituo vya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa dawa, malalamiko yaliyopokelewa na hatua zilizochukuliwa kuyatatua.

Amesisitiza kuwa kila changamoto inayoripotiwa inapaswa kuambatana na jina la mhusika anayeshughulikia suala hilo pamoja na muda wa kukamilisha hatua zilizopangwa. Ameonya dhidi ya kuwasilisha takwimu zisizolingana kwa mamlaka tofauti, akieleza kuwa taarifa sahihi na za uwazi zitasaidia Serikali kupata picha halisi ya utekelezaji.

Katika kuimarisha utoaji wa huduma, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kuboresha matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuwezesha wananchi kutambuliwa, kupata huduma na kufuatilia haki zao bila usumbufu usio wa lazima.

Ameeleza kuwa mzabuni amepatikana kwa ajili ya kupanua matumizi ya mifumo ya kumbukumbu za kielektroniki za wagonjwa (EMR) katika hospitali za ngazi ya juu zilizotajwa kwenye mpango huo, huku mfumo wa GoTHOMIS ukiendelea kutumika katika vituo vilivyo chini ya hospitali za wilaya, ikiwemo vituo vya afya.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA unalenga kuboresha huduma za kila siku, kuhakikisha taarifa za wagonjwa zinapatikana kwa ufanisi na kupunguza usumbufu wanaokutana nao wananchi wanapotafuta huduma za afya.