MHE. MCHENGERWA ATOA MAELEKEZO KUMI NA MBILI KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: October 12th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametoa maelekezo kwa viongozi wa mikoa na halmashauri nchini kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unazingatia sheria, ubora wa huduma na maslahi ya wananchi ili kujenga imani ya kudumu katika mfumo huo.
Ametoa maelekezo hayo leo Oktoba 12, 2026 wakati wa kikao kazi chake na Wakuu wa Mikoa kuhusu ajenda ya Bima ya Afya kwa wote, kilichofanyika jijini Dar es Salaam
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa kila kituo cha kutolea huduma za afya kinapaswa kuwa na maandalizi ya kutosha kabla ya kuanza kutoa huduma kwa wanachama wa bima, yakiwemo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, mifumo ya TEHAMA inayofanya kazi pamoja na utaratibu wa kuendelea kutoa huduma pale mifumo ya kielektroniki inapopata hitilafu.
Amesema kila kasoro inayobainika inapaswa kupewa mhusika wa kuirekebisha na muda usiozidi siku 14, huku changamoto zinazohatarisha maisha au usalama wa mgonjwa zikishughulikiwa mara moja. Ameelekeza kuwa vituo ambavyo havitarekebisha kasoro ndani ya muda uliowekwa viwasilishwe kwa mamlaka husika pamoja na taarifa za changamoto na hatua zilizochukuliwa.
Aidha, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha mahitaji ya dawa yanakadiriwa kwa usahihi na maagizo yanawasilishwa Bohari ya Dawa (MSD) kwa wakati ili kuzuia upungufu wa dawa muhimu. Amesisitiza kuwa fedha zinazopatikana kupitia marejesho ya bima ya afya zitumike kuboresha huduma, ikiwemo ununuzi wa dawa, vifaa tiba na uendeshaji wa huduma kwa mujibu wa taratibu.
Ameeleza kuwa Wizara ya Afya itaendelea kusimamia MSD na kuhakikisha madai sahihi ya vituo vya kutolea huduma za afya yanahakikiwa na kulipwa kwa wakati kwa mujibu wa taratibu na mikataba iliyopo.
Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa mafanikio ya Bima ya Afya kwa Wote yanapaswa kupimwa kwa uwezo wa vituo kutoa huduma bora na salama kwa wakati, badala ya kutegemea takwimu za usajili pekee.