MHE. MCHENGERWA: BIMA YA AFYA KWA WOTE NI MKATABA MKUBWA KATI YA SERIKALI NA WANANCHI
Posted on: October 12th, 2026Na. Clement Robert, WAF - Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote ni dhamana kubwa kati ya Serikali na wananchi inayohitaji ushirikiano na uwajibikaji wa viongozi katika ngazi zote za Serikali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.
Akizungumza hayo wakati wa kikao chake na Wakuu wa Mikoa kuhusu ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote, ninachofanyika jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 12, 2026. Mhe. Mchengerwa amesema mpango huo ni sehemu ya ahadi iliyotolewa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ambayo wananchi waliikubali kwa kutoa kura zao, hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha ahadi hiyo inatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
Amesema utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote hauwezi kufanikiwa kwa juhudi za Wizara ya Afya pekee, bali unahitaji ushirikiano wa karibu wa viongozi na watendaji katika ngazi zote za Serikali. Amewataka viongozi kutumia maarifa waliyoyapata kupitia mawasilisho ya kitaalamu kuandaa mipango ya utekelezaji, kuondoa vikwazo mapema na kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo huo.
Aidha, amesisitiza kuwa Bima ya Afya kwa Wote ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa inagusa maisha ya Watanzania wengi, wakiwemo watoto watakaozaliwa, na kwamba mahitaji ya matibabu hayawezi kusubiri wakati mwananchi anapokabiliwa na ugonjwa.
Ameeleza kuwa tofauti na miradi ya miundombinu inayoweza kukabiliwa na ucheleweshaji, huduma za afya zinahitaji kupatikana kwa wakati kwa sababu ugonjwa hausubiri mwananchi apate fedha za matibabu.
Mhe. Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kila mmoja ana mpango madhubuti wa utekelezaji unaobainisha hatua za kuchukua, wadau wa kushirikiana nao na namna ya kupima mafanikio, akisisitiza kuwa matokeo ya mpango huo yanapaswa kuonekana kupitia huduma bora zinazowafikia wananchi.