Wizara Ya Afya

PROF. SUNGUYA: AZITAKA NCHI ZA AFRIKA KUWEKA MIKAKATI YA KUTOKOMEZA VIFO VYA WAJAWAZITO

Posted on: October 12th, 2026

Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam


Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Bruno Sunguya, amezitaka nchi za Afrika kuimarisha mikakati ya kuzuia na kutibu kuvuja damu nyingi wakati au baada ya kujifungua (Postpartum Haemorrhage – PPH), ili kupunguza vifo vya wajawazito vinavyoweza kuzuilika.


Ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2026, jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe,wakati akifungua warsha ya kikanda kuhusu kinga na udhibiti wa kuvuja damu baada ya kujifungua, warsha hiyo inayowakutanisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 23 za Afrika.


Prof. Sunguya ameeleza kuwa changamoto hiyo inaendelea kuathiri afya ya mama na mtoto kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo kuchelewa kutambua dalili za kuvuja damu, upungufu wa damu salama kwa ajili ya kuongezewa wagonjwa na kutofuata miongozo ya matibabu.


Amesema, kukabiliana na changamoto hiyo ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu, hususan Lengo la 3.1 linalolenga kupunguza vifo vya wajawazito duniani hadi chini ya vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000.


Akizungumzia juhudi za Tanzania, Prof. Sunguya amesema afya ya mama na mtoto imepewa kipaumbele cha kitaifa chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Kinara wa Umoja wa Afrika katika masuala ya afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto.


Ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kuwekeza katika kuimarisha huduma za dharura za uzazi, kuongeza uwezo wa wakunga na kupanua upatikanaji wa teknolojia muhimu za afya, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinahitaji kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ili kuongeza matokeo chanya katika kuokoa maisha ya wanawake na watoto.


Prof. Sunguya amebainisha kuwa warsha ni fursa ya kujifunza baina ya nchi, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika kutatua changamoto zinazofanana, ikiwemo kuimarisha mifumo ya ugavi wa bidhaa tiba na upatikanaji wa huduma bora za uzazi.