TAMISEMI YATOA MAELEKEZO MAHUSUSI KUIMARISHA UTEKELEZAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE.
Posted on: October 12th, 2026Na Clement Robert, WAF - Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Jafari Seif, ametoa maelekezo sita kwa viongozi wa mikoa, wilaya na halmashauri nchini ili kuimarisha utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.
Dkt. Seif ameyazungumza hayo katika kikao kazi cha Waziri wa Afya, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, na Wakuu wa Mikoa kuhusu Bima ya Afya kwa Wote kinachofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 12, 2026.
Dkt. Seif amesisitiza umuhimu wa kusimamia ubora wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya, akiwataka viongozi kuhakikisha wananchi waliojiunga na bima wanapata huduma kwa wakati ili kuongeza imani yao kwa mpango huo na thamani ya fedha wanazochangia.
Amesema changamoto za upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, mashine, vitendanishi vya maabara na watumishi zinapaswa kupewa kipaumbele katika vikao vya usimamizi wa huduma za afya ili kupata ufumbuzi wa haraka.
Aidha, amewataka viongozi wa mikoa na halmashauri kushirikiana na TASAF,mfuko wa NHIF na mamlaka nyingine zinazohusika katika utambuzi, uhakiki na usajili wa wananchi wasio na uwezo, ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Seif ameelekeza Bima ya Afya kwa Wote kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Kamati za Ushauri za Mikoa na Wilaya, ambapo taarifa za maendeleo ya usajili, upatikanaji wa huduma, changamoto na hatua za kuzitatua zitawasilishwa na kujadiliwa.
Amehimiza pia matumizi na uunganishwaji wa mifumo ya TEHAMA, ikiwemo GoTHOMIS na mifumo ya NHIF, ili kurahisisha utoaji wa huduma na uwasilishaji wa madai, akisisitiza umuhimu wa taasisi husika kushirikiana kutatua changamoto zinazojitokeza katika utoaji wa huduma za afya.
Vilevile, amewataka viongozi kuimarisha uratibu na uwajibikaji kwa kushirikiana na halmashauri, mifuko ya bima ya afya, watoa huduma za afya wa umma na binafsi, viongozi wa jamii na dini pamoja na wadau wengine katika kusimamia usajili na utoaji wa huduma.