MHE. CHALAMILA: SEKTA YA AFYA IPEWE KIPAUMBELE KWA USALAMA NA MAENDELEO YA TAIFA
Posted on: October 12th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema sekta ya afya ni nguzo muhimu katika kuhakikisha usalama wa taifa na kukuza uchumi kupitia kuwa na rasilimali watu wenye afya bora na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Akizungumza mbele ya Waziri wa Afya Mhe. Mohammed Mchengerwa, wakati wa kikao kazi cha Mhe. Mchengerwa na Wakuu wa Mkoa kuhusu ajenda ya bima ya afya kwa wote, leo Oktoba 12, 2026, jijini Dar es Salaam , Mhe. Chalamila amesema kuwa uwepo wa rasilimali za kiuchumi pekee hautoshi kuleta maendeleo ikiwa wananchi hawana afya bora inayowawezesha kutumia rasilimali hizo kwa ufanisi. Amesisitiza kuwa afya inapaswa kupewa kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya taifa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutenganisha masuala ya afya na maslahi ya kisiasa, akieleza kuwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unahitaji maamuzi yanayozingatia mahitaji halisi ya wananchi na utayari wa wadau wote kushirikiana.
Ametoa mfano wa Mkoa wa Dar es Salaam, akieleza kuwa pamoja na kuwa na shughuli nyingi za kiuchumi, bado kuna changamoto za uelewa wa wananchi kuhusu wajibu wao katika kuchangia huduma za kijamii. Amesema ni muhimu kujenga utamaduni wa wananchi kutambua umuhimu wa afya zao na kushiriki katika mifumo inayowezesha upatikanaji wa huduma hizo.
Vilevile, Mhe. Chalamila amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za afya kwa wazee, wakiwemo upatikanaji wa dawa na matibabu wanayohitaji. Ameeleza kuwa mafanikio ya Bima ya Afya kwa Wote yatategemea uelewa wa wananchi, usimamizi madhubuti na ushirikiano wa viongozi na wadau wote katika kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi.