WIZARA YA AFYA YAWEKA MIKAKATI YA KUIMARISHA UHAMASISHAJI WA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Posted on: October 12th, 2026Na Aisha Swahibu, WAF - Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia masuala ya Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amesema Wizara itaweka mikakati madhubuti ya kuimarisha uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote, ili waweze kunufaika na huduma za matibabu kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi katika mfumo wa bima ya afya nchini.
Bw. Emmanuel ameyasema hayo leo Oktoba 12, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa Kikao Kazi cha Waziri wa Afya, Mhe. Mohammed Mchengerwa, na Wakuu wa Mikoa kuhusu ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote, kilicholenga kujadili mikakati ya utekelezaji wa awamu ya pili ya uhamasishaji na namna bora ya kuwafikia wananchi katika makundi mbalimbali.
Amesema katika awamu hiyo, ni muhimu kuweka mikakati itakayowahamasisha wananchi kujiandikisha na kulipia bima zao, huku akibainisha kuwa bado kuna changamoto ya kuwafikia baadhi ya wanufaika na kuhakikisha wanachukua kadi zao za bima hata pale ambapo gharama zao zimelipiwa. Hivyo, amewataka viongozi na wadau kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha uhamasishaji na kuongeza mwitikio wa wananchi.
Aidha, amesema Wizara ya Afya itashirikiana na Mikoa kuweka mfumo wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kutumia viashiria muhimu vya utendaji (KPIs), vitakavyosaidia kupima maendeleo ya utekelezaji na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
Amefafanua kuwa takwimu za utekelezaji zitakuwa zikitolewa mara kwa mara ili kuwezesha Wizara na Mikoa kutathmini hatua zilizofikiwa, kubaini changamoto na kuweka mikakati ya kuongeza kasi ya utekelezaji. Mfumo huo utasaidia kuweka malengo yanayopimika na kuimarisha uwajibikaji wa viongozi katika kutekeleza ajenda ya Bima ya Afya kwa Wote.