ZINGATIENI UBORA WA HUDUMA ZA AFYA KWA WANANCHI
Posted on: September 15th, 2023Na. Shaban Juma - Rukwa
Watumishi wa Afya nchini wametakiwa kuzingatia ubora wa huduma za Afya katika Hospitali, Zahanati na Vituo vya Afya ili kuendelea kuboresha huduma za Afya nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mganga mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu akiwa katika ziara Mkoani Rukwa kwa ajili ya kukagua utoaji wa huduma katika Hospitali, Zahanati na vituo vya Afya ikiwa ni maandalizi ya Kampeni ya chanjo ya Polio.
“Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha sana Sekta ya Afya Nchini hivyo ni jukumu letu kuboresha huduma tunazizitoa kwa wananchi”. Amesema Prof. Nagu
Aidha, Prof. Nagu amewasisitiza watumishi wa Afya wazingatie miongozo ya utoaji wa huduma za Afya pamoja na kutoa kauli nzuri kwa wananchi.
“katika kuboresha ubora wa huduma ni lazima tuwe na kauli nzuri, kauli zetu ziwe kauli zenye staha, hata kama mgonjwa amekata tamaa kwa kujua hana muda mrefu wa kuishi, wajibu wako ni kumfanya ajione ana muda mrefu wa kuishi”. Amesisitiza Prof. Nagu
Sambamba na hayo Prof. Nagu ameyashukuru mashirika ya WHO na UNICEF katika kuunga mkono juhudi za kuimarisha Afya za wananchi kwa kushirikiana na Serikali katika kuendelea kutoa huduma.
Hata hivyo, Prof. Nagu amewapongeza watumishi wa Mkoa wa Rukwa kwa kusimamia huduma za Afya kwa ufanisi na umakini wa kutoa huduma na kuendelea kudumisha usafi katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
“Niendelee kuwaomba watumishi wenzangu kushirikiana kwa pamoja katika kuwahudumia wananchi, kwani Serikali imewekeza katika Sekta ya Afya kwa lengo la kuboresha huduma hii, hivyo tukishirikiana kwa pamoja itatusaidia katika kuwahudumia vyema wananchi”. Amesema Prof. Nagu