Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WIZARA YA AFYA YAWASILISHA KWA KAMATI TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2024/25

Posted on: March 20th, 2025

Na WAF - Dodoma

Wizara ya Afya katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/25, iliainisha vipaumbele vilivyozingatia uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa, kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya kuanzia ngazi ya zahanati hadi taifa ili kurahisha upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo Machi 19, 2025 wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Bernadetha Mushashu.

"Pia, Wizara imeimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini, huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika Sekta ya Afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi, huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi," amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri Mhagama amesema, katika kipindi cha utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2024/25 jumla ya akina mama wajawazito milioni 1,846,540 walihudhuria kliniki ambapo kati yao, milioni 1,744,980 sawa asilimia 94.5 walifanya mahudhurio manne ikilinganishwa na asilimia 91 katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita.

Waziri Mhagama amesema Wizara inaendelea kudhibiti kuingia nchini kwa magonjwa hatari yanayoambukiza ikiwemo ebola, marburg, mafua ya ndege, UVIKO-19, homa ya manjano pamoja na homa ya nyani (M-Pox) katika mipaka ambapo kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025 jumla ya wasafiri milioni 1,175,710 waliingia nchini na kufanyiwa uchunguzi wa awali.

Waziri Mhagama ametoa wito kwa wananchi kuendelee kujiunga na mifumo mbalimbali ya bima ya afya ili kupata huduma za afya bila kikwazo cha fedha, kwani hadi sasa asilimia 15 tu ya Watanzania wamejiunga na Mifumo ya Bima za Afya huku asilimia 85 ikiwa nje ya mfumo wa Bima ya Afya.