Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WIZARA YA AFYA YAPOKEA UGENI WA BALOZI WA CUBA NCHINI

Posted on: June 8th, 2022

Balozi wa Cuba nchini Bw. Yordenis Despaigne leo ametembelea Wizara ya Afya kwa lengo la kujitambulisha na kufanya mazungumzo na Mhe. Waziri. Balozi huyo amekutana na Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel katika ofisi za wizara jijini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, balozi huyo amesema Serikali ya Tanzania pamoja na Cuba zimekua na ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa kipindi kirefu hususan upande wa afya ambapo nchi hiyo imekua ikiwaleta madaktari bingwa kufanya kazi nchini.

Balozi Despaigne amesema hivi sasa Tanzania ina madaktari kutoka nchini Cuba wapatao 41 ambapo wanafanya kazi katika Hospitali mbalimbali za Tanzania bara na Zanzibar.

Aidha, Balozi huyo amesema nchini Cuba kuna wanafunzi wa kitanzania takriban 295 huku 186 wakisomea kada mbalimbali za afya na 24 kati yao wanasomea ubobezi.

Akizungumzia utaalam wa Cuba katika mambo ya dawa, balozi huyo amesema Cuba imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa dawa pamoja na chanjo ambapo imeweza kutengeza chanjo 5 za UVIKO-19 huku 3 kati ya hizo zikitumika katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo chanjo ya Watoto kuanzia miaka miwili na kuendelea.

Kwa upande wake Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel amemshukuru balozi Despaigne kwa kuitembelea Wizara ya afya na kumuomba ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo uendelee huku akimuomba kupata uzoefu wa wataalamu katika kutengeneza chanjo ya UVIKO-19 licha ya kuwa imeshaanza.

Dkt. Mollel amesema licha ya Tanzania kupiga hatua katika huduma za afya kusini mwa bara la sahara lakini bado inahitaji kujifunza utaalam na teknolojia kutoka katika mataifa mengine ili kusaidia kutatua changamoto zinaikabili nchi katika upande wa afya. Katika kujibu hilo, Mhe. Balozi amekubali ombi hilo na kusema nchi yake iko tayari kuisaidia Tanzania kupata hiyo technolojia. Ili kufanikisha ombi hilo pande zote zimekubaliana kuanza mazungumzo na kwa upande wa Tanzania kikosi kazi imeundwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya andiko la awali(Concept Note) na kwa upande wa Cuba focal person ni Mhe. Balozi mwenyewe.