Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WIZARA YA AFYA NA DART WAJA NA MKAKATI WA ELIMU KUHUSU MPOX KWA ABIRIA

Posted on: August 24th, 2024

Na. WAF - Dar Es Salaam


Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART), leo Agosti 24, 2024 imetoa elimu juu ya ugonjwa wa Mpox kwa wananchi na abiria kituo cha mabasi hayo kilichopo Mbezi, Jijini Dar Es Salaam. 



Akitoa Elimu hiyo Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya,  Dkt. Jonas Norman  amesisitiza kwamba Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu, hususani maeneo yanayokusanya watu wengi kama vyombo vya usafiri, na kuongeza kuwa ugonjwa huu haujafika nchini lakini ni muhimu elimu ikaendelea kutolewa ili tuwe tayari .


“Dalili za ugonjwa huo ni homa, kutokwa na vipele vyenye maji, uchovu wa mwili, maumivu ya mgongo kuvimba, mitoki ya mwili, maumivu ya misuli, na kuumwa kichwa. Pia ugonjwa huo unaweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine ni kupitia kujamiiana na mtu aliye na ugonjwa huo, kushikana mikono, kupiga/kupigwa busu na mtu mwenye ugonjwa pamoja na kukumbatiana” amesema Dkt Norman


Kwa upande wake Mkurugenzi Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), William Gatambii ameshukuru kwa kupewa mwongozo na Wizara ya Afya katika kutoa elimu ya afya kuhusu Mpox na wataendelea kutekeleza maelekezo yote ikiwemo kuhakikisha vyombo vya kunawia mikono vinarudishwa katika vituo vya abiria.


Wizara ya Afya inaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu huku ikisisitiza wananchi kupiga simu bure kwenda namba 199 kwa msaada na elimu zaidi kuhusu ugonjwa wa Mpox.