Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAZIRI UMMY ASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA ARV KWA WENYE VVU

Posted on: September 7th, 2023

Na. WAF - Dodoma


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesisitiza kuzingatia matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI (ARV) kwa watu wanaoishi na Virusi hivyo ili kuendelea kujilinda na kuwalinda wengine. 


Waziri Ummy ameyasema hayo Septemba 7, 2023 kwenye kilele cha Mdahalo wa Kitaifa wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Tanzania (NACOPHA) uliofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma. 


“Nataka kuwasisitiza watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI ni kuzingatia matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI ili kuweza kujilinda wao wenyewe lakini pia na kuwalinda wengine na ugonjwa huo”. Amesema Waziri Ummy 


Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa Jarida Maarufu la Kimataifa la Sayansi na Afya (Lancet) limethibitisha pasi na shaka ikiwa watu wenye Virusi vya UKIMWI wakitumia vizuri dawa za ARV basi inapunguza maambukizi kwa wengine kwa asilimia zaidi ya 70.


“Kwahiyo niwaombe sana ndugu zangu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI tuendelee kuzingatie matumizi sahihi na endelevu ya dawa za kufubaza Virusi vya UKIMWI (ARV) ili tuwakinge na wenzetu”. Amesema Waziri Ummy