Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAZIRI UMMY AAGIZA HOSPITALI ZA RUFAA ZA MIKOA KUANZA KUTENGENEZA MAZAO YA DAMU

Posted on: June 16th, 2023

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameziagiza Hospitali za Rufaa za Mikoa nchini kuanza kutengeneza mazao ya damu salama ili kuweza kuongeza wigo wa upatikanaji wa plasma kwa ajili ya kuokoa Maisha ya akinamama wajawazito na wenye uhitaji.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo leo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mchangia Damu Duniani Juni 14 2023 ikiwa sambamba na uzinduzi wa Jengo la Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Kati Dodoma lililopo Itega, Jijini Dodoma.

“Serikali imeongeza vituo saba vya kutengenezea mazao ya damu kama vile plasma (Fresh Frozen Plasma-FFP), chembe sahani za damu, na chembe hai nyekundu na kufanya kuwa na jumla ya vituo 15 nchi nzima kutoka vituo saba vya Kanda vilivyokuwa vikitengeneza mazao ya damu kwa mwaka 2021/2022”. Amesema Waziri Ummy.

Waziri ummy ameongeza kuwa licha ya kuwepo vituo hivyo bado havikidhi mahitaji ambapo kupitia vituo hivyo Wizara kupitia Mpango wa Taifa wa damu salama iliweza kukusanya 25,658 za mazao ya damu aina ya Plasma (FFP) ambazo zilitumika kusaidia akina mama wanaopata matatizo ya kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua na chupa 6,625 za chembe sahani (Platelets) zilizotumika kutibu wagonjwa wa saratani, seli mundu pamoja na wagonjwa waliokuwa na matatizo mengine.

Aidha, Waziri Ummy amesema takwimu za ukusanyaji wa damu zimeonesha mafanikio ya kuongozeka kwa ukusanyaji wa damu mwaka hadi mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Mpango umeweza kukusanya chupa za damu 495,600 sawa na asilimia 84 ya mahitaji ya damu nchini ikilinganishwa na chupa 366,206 zilizokusanywa mwaka 2021/2022 sawa na asilimia 67 ya mahitaji.

Mafanikio hayo yamekuja baada ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua jukumu la kununua na kusambaza mifuko ya kukusanyia damu bure nchi nzima na kuhakikisha hakuna upungufu wa mifuko ya kukusanyia damu katika vituo vyote kwa wakati wote.

Kuhusu ufunguzi wa kituo cha Mpango wa Taifa wa Damu Salama Kanda ya Kati Dodoma Waziri Ummy amesema kitasaidia kuboresha huduma za damu salama kwa Mikoa ya Iringa, Singida na Dodoma..