Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WAZIRI MHAGAMA AIONGOZA KANDA YA AFRIKA KUUNGA MKONO VIPAUMBELE VYA WHO

Posted on: May 19th, 2025

Na WAF - Geneva, Uswisi

Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika inaunga mkono vipaumbele vya Shirika la hilo pamoja na juhudi za kuweka mikakati ya kukabiliana na suala la ufadhili endelevu wa kifedha katika mabadiliko yanayoendelea bila kuathiri mshikamano na dhamira ya Shirika hilo.

Waziri wa Afya Mhe. Jenesta Mhagama amesema hayo leo Mei 19, 2025 wakati akiwasilisha taarifa ya Shirika hilo Kanda ya Afrika kwa niaba ya nchi 47 wanachama wa Shirika la hilo Kanda ya Afrika katika kikao cha mapitio ambapo anategemea kuiwasilisha rasmi katika Mkutano Mkuu wa WHO baada ya wasilisho la Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tendros Adhanom Ghebreyesus.

"Kanda ya Afrika inathamini msaada endelevu wa Shirika la Afya Duniani katika kuimarisha mifumo ya afya, kupambana na magonjwa ya kuambukiza, kukuza huduma ya Afya kwa wote pamoja na kudhibiti milipuko ya magonjwa kama vile Marburg, MPOX na kipindupindu," amesema Waziri Mhagama.

Aidha, Waziri amempongeza Dkt. Tedros, pamoja na timu yake kwa uongozi wao imara katika kuimarisha mifumo ya afya Duniani ikiwemo Tanzania ambapo imeweza kupambana na magonjwa ya milipuko.

Kupitia mkutano mkuu huo Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewashukuru Mawaziri wa Afya kutoka nchi 47 wa Kanda ya Afrika kwa kuichagua Tanzania kushika nafasi ya Ukurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, iliyochukuliwa na Profesa Mohammed Yakub Janabi.