Ministry of Health

WAZIRI MCHENGERWA AWATAKA VIONGOZI WA HALMASHAURI KUHAKIKISHA AMBULANCE ZINAKUWA TAYARI MUDA WOTE

Posted on: September 24th, 2026

Na Cletus Sanga, WAF – Kibaha

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha gari la wagonjwa lililokabidhiwa kwa Kituo cha Afya Magindu linatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kuwa tayari muda wote ili liweze kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumza leo tarehe 24 Agosti 2026 katika hafla ya kukabidhi gari hilo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, Mhe. Mchengerwa amesema ambulance hiyo haipaswi kutumika kwa shughuli za kawaida za kiutawala, safari binafsi au matumizi mengine yasiyohusiana na huduma za afya, akisisitiza kuwa ni mali ya umma inayopaswa kutumika kwa kuzingatia uhitaji wa kitabibu bila ubaguzi.

Mhe. Mchengerwa amesema kukabidhiwa kwa gari hilo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha huduma za dharura nchini, ambapo litasaidia kuwafikia na kuwasafirisha kwa usalama wagonjwa na majeruhi wanaohitaji huduma za haraka, wakiwemo wajawazito wenye dharura, watoto wachanga, waathirika wa ajali na wagonjwa wenye hali mbalimbali za dharura.

Aidha, ameitaka Halmashauri kuweka mfumo wa matengenezo kwa mujibu wa maelekezo ya mtengenezaji, akisema kuzuia hitilafu ni nafuu kuliko kusubiri gari liharibike na kuhitaji matengenezo makubwa.

Mchengerwa amesema mafanikio ya huduma za dharura hayatapimwa kwa idadi ya magari yaliyokabidhiwa pekee, bali kwa idadi ya magari yaliyo tayari kufanya kazi, wagonjwa waliofikiwa kwa wakati na maisha yaliyookolewa, hivyo ameitaka Halmashauri kuhakikisha ambulance hiyo inatunzwa, inatumika kwa kusudi lake na inakuwa tayari muda wote.