SERIKALI YAIMARISHA HUDUMA ZA DHARURA KUOKOA MAISHA
Posted on: September 24th, 2026Na Andrea Kadege, WAF – Kibaha
Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha mfumo wa huduma za dharura nchini kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaokumbwa na dharura za kiafya wanapata huduma kwa wakati, hivyo kuongeza uwezekano wa kuokoa maisha.
Akizungumza leo tarehe 24 Agosti, 2026 katika hafla ya makabidhiano ya gari la kubebea wagonjwa (ambulance) wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, amesema huduma za dharura ni miongoni mwa maeneo yanayopewa kipaumbele na Serikali kutokana na umuhimu wake katika kuokoa maisha.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano, kuanzia mwaka 2021, Serikali imeongeza idadi ya vituo vya huduma za dharura nchini kutoka vituo saba (7) hadi kufikia vituo 125, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma hizo kwa wananchi. Mkoa wa Pwani kwa sasa una vituo sita vya huduma za dharura.
Dkt. Sylvanus amesema kuwa uwepo wa mfumo imara wa huduma za dharura, kuanzia wakati taarifa ya tukio inapopokelewa, mwitikio wa timu za dharura, huduma ya awali na usafirishaji wa mgonjwa hadi anapofikishwa katika kituo chenye uwezo wa kutoa huduma stahiki, ni muhimu katika kupunguza vifo na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na kuchelewa kupata huduma.
Aidha, amesisitiza kuwa watumishi wa afya wanapaswa kutoa huduma kwa upendo, huruma, haraka na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, akieleza kuwa kila mgonjwa anayefika katika kituo cha kutolea huduma anapaswa kuhudumiwa kwa wakati na kwa kuzingatia mahitaji yake.
Amesema Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na wadau na viongozi katika kuimarisha huduma za dharura, ikiwemo kuongeza upatikanaji wa vituo, magari ya kubebea wagonjwa na wataalamu wenye uwezo wa kutoa huduma za dharura, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati na kuongeza ufanisi wa mfumo wa huduma za dharura nchini.