Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATUMISHI SEKTA YA AFYA WAMETAKIWA KUENDELEA KUFUATA MIONGOZO YA KIUTUMISHI

Posted on: January 28th, 2024



Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu, Wizara ya Afya Bw. Danny Temba amewataka watumishi sekta ya Afya kuendelea kufuata miongozo na sheria za Kiutumishi iliyowekwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya, kwa kuwa Serikali imewajengea miundombinu bora ya ufanyaji kazi.

Bw. Temba aliyasema hayo Januari 26, 2024 Mkoani Njombe katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi kati ya aliyekuwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Njombe Dkt. Winfred Kyambile na Mganga Mfawidhi wa sasa Dkt. Gilbert Kwesi.

“Hospitali hii ni moja wapo wa hospitali nzuri yenye majengo na mazingira mazuri na yanatia moyo kufanya kazi, mnapaswa kujivunia kwa kufanya kazi katika mazingira mazuri kama haya hivyo mfuate miongozo ya kiutumishi iliyowekwa. Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassani amefanya kazi kubwa sana, hivyo tusimwangushe”. Alisema Bw. Temba.

Pia aliwataka Viongozi wa Hospitali hiyo kusimamia vyema na kutumia mapato ipasavyo na kwa kufuata taratibu za kiserikali, lakini pia kutengeneza mazingira ya kufikiwa na watumishi na wananchi ili kutatua matatizo haraka.

Aidha Bw. Temba alimpongeza aliyekuwa Mganga Mfawidhi, Dkt. Winfred Kyambile kwa kazi kubwa ya usimamizi mzuri wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe pamoja na watumishi wote kwa kuwa sehemu ya mafanikio hayo .

“Rasmi kwa niaba ya Wizara, ya Afya tunampongeza Dkt. Kyambile kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kusimamia vyema ujenzi wa Hospital lakini pia tunatambua pia mchango mkubwa wa watumishi katika ujenzi huo.” Alisema.

Naye aliyekuwa Mganga Mfawidhi Dkt. Winfred Kyambile, amewaomba watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mganga Mfawidhi, Dkt. Gilbert Kwesi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Rufaa mkoa wa Njombe, Dkt. Gilbert Kwesi, aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kumwamini, na kuahidi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuzidi kuboresha utoaji huduma za Afya kwa wananchi.