Customer Feedback Centre

Ministry of Health

WATU 100 WAFANYIWA UPASUAJI WA KUZIBUA MISHIPA YA DAMU YA MIGUU, JKCI

Posted on: July 28th, 2023

Na Mwandishi wetu, JKCI.


Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefanya upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya miguu iliyoziba kwa wagonjwa 100 wenye matatizo hayo kwa kutumia mtambo wa Cathlab kuzibua mishipa hiyo.


Matibabu hayo yamefanyika katika kambi maalumu ya matibabu ya siku tano inafanywa na madaktari bingwa wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na  mwenzao kutoka Hospitali ya BLK iliyopo nchini India.


Akizungumzia kuhusu kambi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema hadi leo tayari wagonjwa 40 wameshapatiwa matibabu na hali zao kuendelea vizuri ambapo baadhi ya wagonjwa tayari wameruhusiwa.


Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu alisema matatizo ya mishipa ya damu ya miguu kuziba yapo kwa wingi katika jamii na mara nyingi huwapata wagonjwa wa kisukari, wagonjwa wa shinikizo la juu la damu pamoja na watu wanaovuta sana sigara na kunywa sana pombe.


“Wagonjwa wengi wenye matatizo ya mishipa ya damu ya miguu kuziba wamekuwa wakikatwa miguu kwa kuchelewa kupata matibabu ama wengine kutokujua tatizo linalowasumbua hivyo kufikia hatua ya kukatwa miguu”, alisema Dkt. Kisenge


Dkt. Kisenge alisema JKCI imeona tatizo la mishipa ya damu ya miguu kuziba linaongezeka kwa kasi hivyo kuamua kuanzisha huduma ya matibabu hayo na kuifanya endelevu kusaidia wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo hayo.


“Baada ya kambi hii madaktari wetu wataendelea kutoa huduma ya matibabu ya mishipa ya miguu baada ya kupata ujuzi kutoka kwa wenzetu wa hospitali ya BLK iliyopo nchini India”, alisema Dkt. Kisenge


Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI inaenda kuanzisha huduma nyingine mpya kwa kushirikiana na mabingwa wa Hospitali ya BLK iliyopo nchini India ya kuzibua mishipa ya damu iliyoziba na kusababisha matatizo ya nguvu za kiume kupungua ili kuwasaidia wagonjwa wanaosumbuliwa na matatizo ya nguvu za kiume.


Kwa upande wake daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu kutoka Hospitali ya BLK iliyopo nchini India Suhail Bukhari alisema hii ni mara ya kwanza wataalamu kutoka Hospitali ya BLK kutoa huduma katika Taasisi hiyo lengo likiwa ni kutoa ujuzi kwa wataalam wa JKCI pamoja na kuwasaidia wagonjwa.