WATANZANIA WATAKIWA KUZINGATIA MTINDO BORA WA MAISHA ILI KUEPUKA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA
Posted on: February 9th, 2024
Na. WAF - Zanzibar
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameendelea kuwasisitiza wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kuepuka magonjwa Yasiyoambukiza kwa kuwa takwimu za 2012 zinaonesha Watanzania 9 kati ya 100 wana Kisukari huku Watanzania 26 kati ya 100 wana Shinikizo la Juu la damu (Presha).
Waziri Ummy amesema hayo leo Februari 9, 2024 kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la ‘Heart Team Africa’ lililofunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango Mjini Zanzibar.
“Kulingana na Utafiti wa STEPs wa WHO za Mwaka 2012 (tunaposubiri data za 2022 kutolewa hivi karibuni) zineonesha kuwa Watanzania 9 kati ya 100 wana Kisukari huku Watanzania 26 kati ya 100 wana Shinikizo la Juu la damu .” Amesema Waziri Ummy
Amesema, katika vitu vya kuzingatia ni pamoja na kupunguza matumizi ya sukari, chumvi, mafuta kidogo, kuacha matumizi ya tumbaku, unywaji pombe uliopitiliza, kuongeza kasi ya mazoezi ya mara kwa mara ikiwemo mazoezi ya viungo.
Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwa kuboresha matibabu ya moyo nchini na upande wa majengo, kuwa na Vifaa Tiba vya kisasa vinavyofanana na vilivyopo nchi zilizoendelea pamoja na kuwaendeleza wataalamu wa moyo kuwa mabingwa wabobezi.
“Serikali imetupa fedha kiasi cha Tsh: Bilioni 9 kwaajili ya kusomesha madaktari kuwa mabingwa wabobezi katika masuala ya moyo na hii itahusisha wataalamu wa Afya ambao ni madaktari wa upasuaji, wauguzi, wafamasia, na madaktari wa usingizi.” Amesema Waziri Ummy
Pia, Waziri Ummy amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepata mafanikio makubwa katika Sekta ya Afya, hivyo inaendelea na juhudi za kuokoa maisha ya Watanzania wenye magonjwa Yasyoambukiza ikiwemo kutoa matibabu na elimu.
“Tunaona fahari kubwa kwa yote ambayo tumefanikiwa katika vituo vyetu vya huduma za Afya ikiwemo kutoa huduma ya hali ya juu nchini Tanzania kama vile Upandikizaji wa Valve ya mishipa kwenye taasisi ya JKCI, Upasuaji wa ‘Transcatheter’ kwa kutumia Angio Suite katika Taasisi yetu ya Kitaifa ya Mifupa.” Amesema Waziri Ummy
Mkutano huo umeangaziwa na mada mbalimbali ambazo zitajadiliwa hapo ni pamoja na namna ya Uchunguzi wa upigaji picha, Upasuaji wa Mishipa, Urekebishaji wa viungo, Uuguzi na Kinga ambapo majadiliano hayo muhimu yatapelekea kubadilishana uzoefu kati ya wajumbe wote waliyopo.