WATAKIWA KUZINGATIA MIONGOZO YA SARATANI YA MACHO
Posted on: May 15th, 2025
Na WAF - KILIMANJARO
Viongozi wanaosimamia Sekta ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kamati za Huduma za Afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri wameagizwa kuhakikisha Mwongozo wa Utambuzi na Tiba kwa Wagonjwa wa Saratani ya Macho na Mwongozo wa kufundishia Afya Msingi ya macho katika vituo vya afya na zahanati inasimamiwa ipasavyo ili kuinua uelewa wa wataalam wa Afya wa kuwatambua watoto wenye changamoto na kuwapa rufaa mapema.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametoa maelekezo hayo Mei 15, 2025 Mkoani Kilimanjaro akiwakilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Jairy Khanga katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Saratani ya macho kwa watoto, yaliyofanyika Katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCMC.
Amesema ni muhimu kuhakikisha miongozo inasimamiwa ipasavyo kwakuwa inaelezea taratibu za ngazi za rufaa za kufuatiliwa ili mtoto asicheleweshwe kwenye kituo cha tiba.
“Ninaelekeza viongozi wa Wizara ya Afya na wale wanaosimamia sekta kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Kamati za Huduma za Afya ngazi ya mkoa na halmashauri kuhakikisha miongozo inasimamiwa ipasavyo, pamoja na kuboresha huduma za afya ili kuwa na vituo vingi zaidi vya kutibu saratani ya retina,”amesema Dkt. Khanga.
Ameongeza kuwa Wizara ya Afya imetoa Mwongozo wa utambuzi na tiba kwa wagonjwa wa saratani ya macho na wa kufundishia afya msingi ya macho katika vituo vya afya na zahanati ili kuinua uelewa wa wataalam wa Afya wa kuwatambua watoto wenye tatizo hili na kuwapa rufaa mapema.
Pia ametoa wito kwa waganga wafawidhi kuhakikisha watumishi kwenye maeneo yao wanapatiwa mafunzo stahiki ili kuharakisha rufaa za wahisiwa wa saratani ikiwemo saratani ya Retina.
Aidha, ameelekeza huduma za uchunguzi wa saratani za retina zijumuishwe kwenye huduma za uangalizi wa maendeleo ya ukuaji wa mtoto na taarifa za uchunguzi zijumuishwe na kufuatiliwa kupitia kadi ya maendeleo ya mtoto.
“Nitumie fursa hii kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuiwezesha Wizara kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma na kuwezesha upanuzi wa huduma hizi kwenye maeneo mengi zaidi,” amesema Dkt. Khanga.